MCHUNGAJI
wa Kanisa la Ufufuo na Uzima jijini Mwanza, Samson Gwajima na Ofisa wa
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Amin Neigwa,
wamevamiwa na majambazi ambao wamewajeruhi vibaya kwa kuwakata mapanga
vichwani.
Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana katika Mtaa wa Lyila, Kata ya Buhongwa, Wilaya ya Nyamagana, jijini Mwanza.
Akizungumza
kwa taabu na mwandishi wetu akiwa wodini kwenye Hospitali ya Rufaa ya
Bugando (BMC), alikolazwa kwa matibabu, Neigwa, alisema akiwa sebuleni
nyumbani kwake na mkewe, ghafla walimuona msichana wa kazi aliyekuwa nje
akichota maji, akiingia ndani kwa kasi na kukimbilia chumbani.
Alisema
wakati akitahamaki kilichotokea, watu wanaosadikiwa kuwa majambazi
waliingia ndani wakiwa na silaha za jadi kama mapanga, nyundo, vitu
vyenye ncha kali na kutaka fedha.
"Walikuwa
sita na baadhi yao walifunika sura zao kwa vitambaa, walinitaka niwape
pesa...nilipata ujasiri wa kumrukia mmoja wao aliyekuwa na panga na
kumkaba ndipo wengine wakanishambulia kwa kutumia silaha zao hadi
nikapoteza fahamu," alisema.
Aliongeza
kuwa, wakati wanamshambulia wengine walikuwa wanamlazimisha mkewe awape
pesa lakini aliwakatalia na baadaye aliamua kuwapa sh. 10,000 ambayo
ilikuwepo wakaichukua.
"Kelele nilizopiga wakati tumevamiwa zilisikika kwa majirani ambao walijitokeza ndipo wavamizi wakakimbia," alisema Neigwa ambaye alijeruhiwa kichwani ambapo hadi jana alikuwa akitokwa na damu masikioni.
Baada
ya watu hao kukimbia, walienda kuvamia nyumbani kwa Mchungaji Gwajima
na kumjeruhi kichwani kwa panga ambapo hivi sasa amelazwa katika
hospitali hiyo kwenye Chumba cha Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalumu
(ICU).
Mchungaji
Gwajima ni kaka wa Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu
Josephat Gwajima, ambaye alivamiwa alipokuwa amelala na familia yake
eneo la Lyila na kulazimishwa kutoa fedha.
Akizungumza
na mwandishi wetu, Mchungaji wa kanisa hilo, John Kiula, alisema
Mchungaji Gwajima alivamiwa usiku ambapo baadhi ya mashuhuda walidai
baadhi ya meno yake yameng'oka.
"Hadi sasa bado hajajitambua, tumetoka kwenye kipimo cha CT-Scan lakini majibu bado hatujapewa tumeambiwa yakiwa
tayari watatujulisha," alisema Mchungaji Kiula.
Mkuu
wa Idara ya Dharura hospitalini hapo, Dkt. Derick David, alikiri
kuwapokea majeruhi hao usiku na kusema Mchungaji Gwajima alifikishwa
akiwa na hali mbaya zaidi kuliko Neigwa.
"Gwajima
ana jeraha kubwa kwenye paji la uso ambalo ni kama sentimita mbili hadi
tatu kwa urefu kwenda ndani, kipimo cha X-Ray kimeonesha hajapasuka
mfupa ila hali yake si nzuri.
"Hadi
sasa bado hajitambui, tunatarajia kumfanyia kipimo kikubwa cha CT-Scan
ambacho kitaonyesha ameumia kiasi gani lakini Neigwa anaendelea vizuri
ingawa naye anahitaji kupimwa na CT-Scan ili kuona majeraha yake kama
amepata athari ndani ya kichwa, tunaendelea kuokoa maisha yao," alisema.
Kamanda
wa Polisi mkoani humo, Naibu Kamishna wa Polisi, Charles Mkumbo,
alikiri kutokea kwa matukio hayo na kuahidi kuyatolea ufafanuzi ambapo
baadhi ya watu wamekamatwa wakihusishwa na matukio hayo.
"Mkuu
wa Upelelezi Mkoa na timu yake walikuwa wanaendelea na uchunguzi,
wakiukamilisha nitalizungumzia kwa undani na kuwataja walioshikiliwa,
baadhi ya majambazi hao wametambuliwa na majirani," alisema.
No comments:
Post a Comment