SERIKALI
ya Comoro imeiomba Serikali ya Tanzania iisaidie kutatua changamoto ya
uhaba wa ndege zinazotua nchini humo hali iliyosababishwa na kusitishwa
kwa huduma za safari za shirika la ndege la Yemen.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julias Nyerere jijini Dar es Salaam, Waziri wa Uchukuzi wa Comoro,
Bahia Masoundi, alisema Shirika la Ndege la Yemen lilisitisha huduma
zake kufuatia machafuko yanayoendelea nchini Yemen.
“Mchafuko
ya nchini Yemen yalipelekea shirika lao la ndege kusitisha huduma zake
na kutokana na kwamba ndilo shirika tulilokuwa tukilitegemea kwa kiasi
kikubwa ndio maana uhaba umejitokeza baada ya kufunga huduma zao,” alisema Massoundi.
Alisema
kwa sasa kuna mashirika manne tu yanayofanya kazi nchini humo na ndege
zinazotua ni chache na kwamba serikali ya nchi hiyo haimiliki shirika
hata moja hivyo kulazimika kuomba msaada nchini Tanzania.
Naye
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Anga Tanzania (TCAA), Charles
Chacha alisema waziri huyo amefanya mazungumzo na waziri wa Uchukuzi
nchini, Samweli Sitta ambaye ametoa maagizo kwa TCAA ili ifanye
utaratibu wa kuisaidia nchi hiyo.
“Tayari
tumepokea maagizo ya Waziri mwenye dhamana na sisi kama mamlaka
inayosimamia safari za anga tunaanza mara moja kuangalia namna ya
kuisaidia Comoro kwasababu ni nchi ambayo ina makubaliano ya kusaidiana
na Tanzania,” alisema Chacha.
Alisema
kwa sasa ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) hufanya safari zake
mara nne kwa wiki nchini Comoro lakini bado kuna tatizo la mrundikano wa
abiria wanaotaka kusafiri kwenda au kuja nchini kwa shughuli za
biashara, utalii au kufuata huduma.
Aliongeza
kutokana na uwezo mdogo wa ATCL atakutana na uongozi wa mashirika yenye
uwezo yanayofanya kazi nchini yaweze kufanya safari nchini Comoro
pamoja na kutoa kibali maalumu kwa shirika la ndege la Ethiopia ili
ndege zake ziende nchini humo baada ya kutua Tanzania.
No comments:
Post a Comment