Hospitali ya AMI Yafungwa Rasmi - LEKULE

Breaking

23 May 2015

Hospitali ya AMI Yafungwa Rasmi

HATIMAYE Hospitali ya African Medical Investment Ltd (AMI) maarufu kama Trauma Center ya Masaki Dar es Salaam, imefungwa rasmi na mmiliki wa jengo kukabidhiwa funguo zake.
 
Hospitali ya AMI na ya gharama ya juu  ilikuwa ikitoa matibabu kwa viongozi wa ngazi za juu wa Serikali, wabunge , mabalozi na wafanyabishara wakubwa wa ndani na nje ya nchi.
 
Kufungwa kwa hospitali hiyo kumetokana na kushindwa kulipa kodi ya pango kwa zaidi ya miezi 26, inayofikia zaidi ya dola za Marekani milioni 1.6, ambazo ni zaidi ya Sh bilioni tatu.
 
Makabidhiano hayo yalifanyika jana hospitalini hapo kati ya Mwakilishi wa Kampuli ya udalali wa Mahakama ya MEM Auctioneers and General Brokers Ltd, Elieza Mbwambwo kwa Meneja wa jengo hilo, Zurfiq Hassanar, dalali huyo wa mahakama alisema hatua hiyo ya kuhamishwa kwa hospitali hiyo imetokana na uamuzi wa Mahakama Kuu.
 
“Ninapenda kusema leo (jana), tunakabidhi jengo na funguo zake kwa Meneja wa jengi hili kwa niaba ya mteja wetu, wiki mbili zilizopita tulikamata mali  baada ya AMI kushindwa kulipa deni kama ilivyoamriwa na mahakama.
 
“Mahakama Kuu ilichoamuru mali za AMI zikamatwe na kupigwa mnada  ili kuweza kulipa deni lao la pango na kisha kuondolewa kwenye jengo na kumkabidhi mmiliki  wake Navtej Singh Bains,” alisema Mbwambo.
 
Mali zilizokamatwa ni magari matatu ya kubebea wagonjwa (Ambulance), vitanda maalumu vya kulaza na kuwahudumia wagonjwa, gari ndogo aina ya Mark II, mashine mbalimbali pamoja na samahani zilizokuwa zikitumiwa katika jengo hilo.
 
“Tulipokuja awali tulitoa taarifa kwa ndugu wa wagonjwa wawe wamewaondoa wagonjwa wao na sasa jengo ni nyeupe halina mtu ndani, hata mali tilizokamata tutazipiga manda ingawa tunajua haziwezi kufikia thamani ya fedha zinazodaiwa, maana kwa sasa kuna maombi mengi ya watu wanataka kufungua hospitali hapa,” alisema
 
Alisema mashine za CT -Scan, X-ray ni miongoni mwa zitakazopigwa manda huku atakayepanga katika jengi hilo akipewa kipaumbele cha kwanza.
 
Hatua hii ya kufukuzwa kwenye jengo imefikiwa baada ya mabishano ya muda mrefu ya kisheria baina ya AMI na mfanyabiashara ambaye pia ni mmiliki wa jengo hilo, Navtej Singh Bains. 
 
Taarifa zaidi inasema kwamba akaunti za Benki za Hospitali hiyo ya AMI katika Benki ya EXIM zilizoambatanishwa na Mahakama zilikutwa zikiwa zimefungwa na fedha zote zikiwa zimetolewa.

Amri ya kufurushwa kwa AMI ilitolewa Mei 7, mwaka huu na kusainiwa na Makamu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania. 
 
Ofisa Mtendaji Mkuu wa AMI Plc, Theunis Peter Botha, ambaye pia ni Mkurugenzi na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya AMI Tanzania, aliwasilisha ombi Mahakama Kuu ya Tanzania kuwa imefilisika.
 
Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wenzake hospitalini hapo, Rose Sesoa, alisema pamoja na kufungwa kwa hospitali hiyo hivi sasa hawajui hatima yao.
 
“Tunaiomba Serikali ichukue hatua sasa.Wakija wawekezaji wageni wawabane kwa maswali maana leo hili limetokea na hapa tupo Staff zaidi ya 100 hatujui tufanye nini. Kikubwa  ni makato ya NSSF ambayo imekuwa ikituma watu wake lakini wakifika hapa wanapewa bahasha na kunyamaza huku Makato hayapelekwi,” alisema Sesoa.
 
AMI Tanzania inamilikiwa na Kampuni mama ya AMI Plc ya London ambayo iliondolewa kwenye Soko la Hisa la London mnamo Februari 2014 baada ya jaribio la kuuza mali zake zilizopo nchini Maputo bila kibali kutoka kwa wanahisa.
 
Pia kumbukumbu zinazoonyesha kuwa Lancet Laboratory (T) Ltd iliwasilisha ombi la dharura dhidi ya kufungiwa kwa Hospitali ya AMI ikiwa inaidai hospitali hiyo zaidi ya Sh  milioni 150.
 

Hata hivyo wakati inafungwa hospitali hiyo, baadhi ya wazabuni walikuwa hospitalini hapo huku wakiwa hajui la kufanya juu ya hatima ya malipo yao.

No comments: