Fidia Kwa Waathirika wa Mafuriko Dar: John Mnyika Amvaa Waziri Mkuu Mizengo Pinda - LEKULE

Breaking

23 May 2015

Fidia Kwa Waathirika wa Mafuriko Dar: John Mnyika Amvaa Waziri Mkuu Mizengo Pinda

MBUNGE wa Ubungo John Mnyika amemshukia Waziri mkuu Mizengo Pinda na kumtaka kuhakikisha kwamba kiasi cha fedha cha Bilioni tatu zitakazotolewa na mfuko wa maafa zinatolewa kwa wakati ili kutatua changamoto za waathirika.

Mbali na hilo amemtaka Rais Kikwete pamoja na Waziri Pinda kumfuatilia Waziri wa Ujenzi John Magufuli kwani alisema mfuko wa barabara umetoa milioni 10 kwa kila Manispaa lakini hadi kufikia sasa fedha hizo hazijaonekana.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana Mnyika alisema hatua zote zitaweza kuongeza kasi zaidi endapo fedha hizo zitapatikana kwa wakati.

Alisema taarifa ya Waziri Pinda kuhusu maafa aliyosema ameipata haikuwa inajitosheleza kwani yapo mambo ya msingi  kwenye maeneo yaliyokubwa na maafa hayakuzingatiwa.

“Taarifa ya Waziri Pinda aliyosema ameipata kuhusu mafuriko haikuwa imejitoshelaza na hili nililibaini baada ya kuzunguka katika Kata 12 kati ya 14 za jimbo la Ubungo,”alisema Mnyika.

Alisema kwa upande wa Jimbo wameshakaa kikao cha mfuko wa maendeleo na kutenga fedha kwa ajili ya maafa.

“Kikawaida jimbo kwa mwaka linakusanya miliono 69 ambapo kati ya hizo asilimia 10 zitaenda kusaidia maeneo yaliyokubwa na maafa ikiwemo Mburahati kuzibua mifereji iliyoziba ,”alisema Mnyika.

Hata hivyo Mnyika aliendelea kusema kuwa katika kuhakikisha kwamba miundombinu iliyoharibiwa na mvua inakarabatiwa upande wa barabara za lami zilizoathirika iangalie wakandarasi wa kwenda kuziba sehemu zilizoharibiwa.

Alisema pia barabara za changarawe wazabuni na wahandisi waagizwe ili kufanya tathimini katika maeno husika ili yaweze kukarabatiwa kwani wananchi wanateseka sana.

Alisema kwa upande wa manispaa ya Kinondoni wametenga kiasi cha Sh milino 10 ambazo zitatolewa kwa awamu kwa kila Kata ili ziweze kusaidia kuboresha miundombinu ya barabara zilizoharibiwa kipindi cha mvua.

Natambua kwamba kuna baadhi ya wananchi kuanzia sasa wameanza kuchanga fedha ili kuhakikisha kwamba wanaboresha mindombinu yao ikiwemo Kata ya Sinza ni wakati wa kuunganisha nguvu za pamoja ili kuweza kufikia malengo,”alisema Mnyika.

Hata hivyo alisema wakati akizunguka katika Kata 12 za Jimbo hilo alibaini kuwa shirika la Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam(DAWASCO) hawajaweka wazi kwani wananchi hawapati maji kama ratiba ilivyopangwa hivyo wamekuwa wakitegemea maji ya Mvua.

Kufuatia hali hiyo aliitaka DAWASCO kuzunguka katika maeneo mbalimbali ili kuona adha wanayopata wananchi na sio kukaa maofisini.

“Kitu cha kuhoji ni kwamba kwanini Bomba la gesi kutoka Mtwara limekamilika kwa wakati lakini miradi hii ya maji ambayo ipo ndani ya jiji la Dar es Salaam haikamiliki kwa kipindi kinachotakiwa ?,”alihoji Mnyika.

Aidha alisema Rais Jakata Kikwete bado hajatekeleza ahadi za wananchi kwani wakati anazindua Daraja la Golani aliahidi Wananchi kuwa ataitisha kikao kujadili masuala hayo na hakutekeleza hadi kufikia sasa.

Alisema ili asije akaondoka na udhaifu huo ni vyema aitishe kikao hicho na yeye ataendelea kubaki Dar es Salaam ili kujadili masuala hayo ya msingi.

“Ahadi za Rais bado hazijatekelezwa wakati akitoa tamko linatekelezwa, lakini tunaona fedha za ufisadi zinapatika ila za miradi ya maendeleo hazipatikani,”alisema Mnyika kwa uchungu.

Alipoulizwa kuhusu kugawanywa kwa majimbo alisema kuwa hakubaliani na hali hiyo kutokana na kwamba inaiongezea gharama kwa Serikali.

Mbali na hilo aliwataka wananchi kuhudhuria baraza la Madiwani Kinondoni leo ambalo litakuwa linajadili suala hilo na waweze kutoa maoni yao.


No comments: