BVR malalamiko kila kona Lindi - LEKULE

Breaking

18 May 2015

BVR malalamiko kila kona Lindi

Dar/Nachingwea.
Wakati uandikishaji wapigakura ukiendelea kulalamikiwa katika Mkoa wa Lindi kutokana na kasoro mbalimbali, madudu zaidi yamebainika, huku Chama cha Wananchi (CUF) kikiitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuweka hadharani idadi ya watu wanaoandikishwa katika kila kata.
Miongoni mwa kasoro zinazolalamikiwa ni pamoja na vituo vya kujiandikisha kuwa tofauti na vile vya kupigia kura na mashine za Biometric Voter Registration (BVR) kuondolewa kabla ya watu kujiandikisha.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema jana kuwa idadi ya watu waliondikishwa katika kila kata ikiwekwa wazi na NEC itawasaidia kulinganisha na makadirio ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ili kufahamu idadi ya watu wasioandikishwa.
Alisema viongozi wa chama hicho walifanya ziara mikoa Ruvuma, Lindi na Mtwara na kushuhudia kasoro nyingi katika uandikishaji.
Akitoa mfano, alisema katika Kata ya Matemanga wilayani Tunduru, asilimia 60 ya watu wenye haki ya kupiga kura hawajaandikishwa, lakini mashine zimehamishwa.
Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva alisema kila aliyefika kwenye kituo cha kuandikisha aliandikishwa.
“Niko Mtwara kutembelea vituo, ninachoweza kusema ni kwamba tume haimfuati mtu nyumbani kwake kwenda kumwandikisha, kila aliyefika kituoni aliandikishwa, sehemu zote tunazopita hakuna malalamiko, sijui akina Lipumba wanapata wapi taarifa hizo, mambo mengine siwezi kuyazungumza kwa sasa,” alisema.
Akifafanua, Profesa Lipumba alisema maeneo mengi waliyotembelea waandikishaji waliopatiwa mafunzo na NEC hawafanyi kazi hiyo kwa sababu ya ufinyu wa bajeti na kwamba kila kituo kina waandikishaji wawili.
“Hata waandikishaji hao wawili katika kila kituo wanalipwa Sh100,000 kwa wiki wakiwa ugenini, posho hii ni ndogo,” alisema.
Katika wilaya ya Nachingwea, uandikishaji kwenye Daftari la Wapigakura ulisimama jana katika vituo 12 kati ya 14 vya kata za mjini Nachingwea kutokana na kasoro za kimfumo, ambapo mashine hizo zilikuwa zinasoma vituo tofauti na mahali vilipo.
Baadhi wa wananchi ambao walijiandikisha jana waliilaumu Tume hiyo kwa kukosa umakini katika utendaji wake.
Mkazi wa Mtaa wa Ugogoni, Athumani Hemed ambaye alijiandikisha katika Kituo cha Walimu (TRC), amepata kitambulisho kinachoonyesha ameandikishwa katika kituo cha Shule ya Msingi Mianzini.
Alisema licha ya kutakiwa kurejesha vitambulisho hivyo leo, huenda idadi ya watakaorudisha ikawa ndogo kwani wengine walishaondoka nje ya maeneo yao.
Ofisa Uandikishaji Msaidizi wa Wilaya ya Nachingwea, Boniface Chatila amekiri kuwapo kwa tatizo hilo ambalo limeathiri vituo 12 kati ya 14.
Nasoro Ndunguru mkazi wa Mtaa wa Ugawaji, ambaye alijiandikisha kwenye kituo cha Shule ya Msingi ya Majengo na kitambulisho chake kuonyesha kuwa ameandikishwa Kituo cha  Sekondari ya Nambambo, aliitaka Tume kuwa makini katika utendaji wake ili kuwapa imani wananchi katika mchakato mzima wa uchaguzi.
 Akizungumzia kasoro nyingine za zoezi hilo, Musa Selemani mkazi wa mtaa wa Ngwea mjini Tunduru alisema baadhi ya vituo vipo maeneo ya mafichoni hali inayosababisha wananchi kushindwa kuvitambua.
Alidai kuwa licha ya wilaya kupeleka marekebisho ya vituo NEC tangu mwaka jana lakini hawajarekebisha hasa maeneo ya mjini. Alisema wamepeleka taarifa hizo Tume na wamedai watarekebisha muda wowote na kwamba shughuli hiyo inaweza kuendelea tena kesho.

No comments: