Urais wawagonganisha NCCR-Mageuzi, Chadema - LEKULE

Breaking

18 May 2015

Urais wawagonganisha NCCR-Mageuzi, Chadema


Dar es Salaam.
Chama cha NCCR-Mageuzi kimeponda kauli ya Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu kwamba Katibu mkuu wa chama hicho kikuu cha upinzani, Dk Willibrod Slaa ndiye atakayekuwa mgombea urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Akiwa kwenye mkutano wa hadhara wa Chadema mjini Moshi, hivi karibuni, Lissu alikaririwa akieleza kuwa Dk Slaa, ndiye atakayepitishwa na Ukawa kugombea nafasi hiyo.
Lakini Mkuu wa Idara ya Kampeni na Uchaguzi wa NCCR-Mageuzi, Faustine Sungura aliliambia gazeti hili mwishoni mwa juma kuwa ni makosa kudhani kwamba Chadema ndicho chenye nafasi ya kusimamisha mgombea urais kupitia Ukawa, wakati bado mchakato wa kumpata mgombea haujafanyika.
Sungura ambaye pia ni miongoni mwa waasisi na mwanzilishi wa mageuzi nchini, alisema kati ya vyama vinne vilivyounda Ukawa, tayari Chadema imepewa majimbo mengi ya ubunge. “Fursa hiyo pekee imeshawapa uwezekano wa kutoa waziri mkuu kama upinzani utashinda”, alisema.
“Kwa kawaida chama chenye wabunge wengi ndicho kinachotoa waziri mkuu, sasa kwa namna yoyote Chadema ndiyo itakayotoa waziri mkuu, hivyo haiwezekani watoe na mgombea urais. Nawashauri wachague nafasi mojawapo,” alisema Sungura.
Sungura alisema kauli hiyo ya Lissu siyo sahihi na hailengi kujenga Ukawa, bali kuubomoa kwa kuwa haiwezekani chama kimoja kitoe rais, makamu wake na waziri mkuu. “Ni vizuri ikaeleweka mapema kwamba, haiwezekani chama kimoja kati ya vyama vinne washirika wa Ukawa, kikatoa mgombea urais, makamu na waziri mkuu,” alisema Sungura  na kuongeza:
“Kwa kuwa CUF kina nafasi kubwa ya kumtoa mgombea urais wa Zanzibar, vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema na NLD, kimoja kati ya vyama hivyo kitamtoa ama rais au waziri mkuu au spika wa Bunge, kinyume chake ni tamaa inayoweza kuua Ukawa.”
Kwa mujibu wa Sungura, mageuzi chanya hayawezi kuletwa kwa ubinafsi, bali nia ya dhati ya Ukawa katika kuyatafuta.

No comments: