Wanawake Pwani Wadaiwa Kuwarubuni Wavulana - LEKULE

Breaking

9 Apr 2015

Wanawake Pwani Wadaiwa Kuwarubuni Wavulana



Wanawake wenye umri mkubwa wametakiwa kuacha kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi na vijana wenye umri mdogo, kwani jambo hilo linawapunguzia heshima katika jamii.

Ushauri huo ulitolewa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Halima Kihemba wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Afya Duniani yaliyofanyika eneo la Kituo cha Afya Mlandizi, wilayani Kibaha mkoani Pwani.

Kihemba, ambaye kitaaluma ni mwanahabari, alisema kuna ripoti za kipolisi mkoani Pwani zinazoeleza kuna kinamama ambao tayari wamevuka umri wa miaka 60 wana uhusiano wa kingono na vijana wenye umri mdogo, jambo linalowapunguzia heshima katika jamii.

“Kuna taarifa kuwa miongoni mwenu kuna kina mama wana tabia mbaya ya kuwa na wapenzi ambao ni vijana wadogo sana kiumri. Kweli si kweli?" Aliuliza mkuu huyo wa wilaya na wazee hao ambao kwa idadi walikaribia 300, wakaitikia ‘Kweliiiii’.

Baadaye, Mwandishi alimfuata Kihemba na kumwuliza juu ya ukubwa wa tatizo hilo mkoani humo ambapo alijibu; “Halijawa tatizo kubwa sana, lakini kuna wachache walio na tabia hizo mbaya, ndio maana tunaanza kulidhibiti ili lisisambae kwa kasi maeneo mengine.”

Alisema tatizo hilo kwa ukubwa lipo miongoni mwa wanaume ambao wamekuwa wakijihusisha na ndoa za utotoni kwa muda mrefu, huku likilazimisha wanafunzi wa kike kukatisha masomo yao kuolewa.

Uchunguzi uliofanywa miongoni mwa wazee ambao walikuwa wanapata huduma ya bure ya kupima afya zao kwa msaada wa shirika lisilo la kiserikali la The Good Samaritan Social Services umethibitisha ubakaji na ndoa za utotoni ni matatizo makubwa maeneo ya Mlandizi na viunga vyake.

Mkurugenzi wa Shirika hilo, Elisha Mwamkinga alisema shirika lake linajitahidi kuwaelimisha wazee kuishi kwa heshima katika jamii na kuepuka mambo ya aibu miongoni mwao.

Kwa ufadhili wa Shirika la HelpAge International, zaidi ya wazee 300 wa Mlandizi walipima afya zao, na wengi wao wakapongeza juhudi zinazofanya na shirika hilo katika kuwapa huduma mbalimbali za kiafya na chakula.

No comments: