Kesi ya kushawishi wafanyabiashara wasilipe kodi kwa serikali inayomkabili Mwenyekiti wa Jumuia ya Wafanyabiashara Nchini, Johnson Minja inaanza kusikilizwa leo.
Kesi hiyo iko katika Mahakama ya Wilaya ya Dodoma Mjini mbele ya Hakimu Mkazi, Rebecca Mbilu ambapo leo itaanza usikilizwaji kwa mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali ya kesi yake.
Mshitakiwa huyo ambaye yuko nje kwa dhamana anakabiliwa na mashtaka mawili ikiwemo la kuchochea wafanyabiashara wasilipe kodi ya serikali.
Upande wa mashtaka kuiongozwa na Wakili wa Serikali, Godfrey Wambali ulidai kuwa, Septemba 6, mwaka jana wakati Minja alipokuwa katika mkutano na wafanyabiashara uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Mipango Mjini hapa mshitakiwa alitenda makosa mawili ya kushawishi wafanyabiashara wasilipe kodi na kuzuia ukusanyaji wa kodi kwa kutumia mashine za kielektroniki (EFDs).
Upande wa mashtaka ulidai kitendo alichofanya mshtakiwa ni kinyume na kifungu cha 390 kinachosomeka pamoja na kifungu cha 35 cha Sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 ni kosa kushawishi vitendo vyovyote vya jinai.
Alidai hata kifungu cha 107 kifungu kidogo cha Sheria ya kodi sura ya 332 ya mwaka 2004 ni kosa kuzuia ulipaji wa kodi kwa Serikali. Mshitakiwa alikana mashtaka hayo. Minja anatetewa na wakili wa kujitegemea Godfyey Wasonga.
No comments:
Post a Comment