Polisi Yazuia Wafuasi Wa Askofu Gwajima.....Vikosi vya Mbwa, Farasi,Magari sasa kila Kona. - LEKULE

Breaking

9 Apr 2015

Polisi Yazuia Wafuasi Wa Askofu Gwajima.....Vikosi vya Mbwa, Farasi,Magari sasa kila Kona.



Jeshi la polisi kanda maalumu ya Dar es salaam limesema wafuasi wa Askofu mkuu wa kanisa la ufufuo na uzima,Josephat Gwajima wasithubutu kutia mguu eneo atakalohojiwa askofu huyo.

Kauli ya jeshi hilo imekuja siku chache baada ya Askofu Gwajima kuwataka wafuasi wake kumsindikiza leo kituo cha polisi kanda maalumu ya Dar es salaam ambako anahitajika ili kuhojiwa.

Msimamo huo ulitolewa jana na kamishna wa polisi katika kanda hiyo, Suleiman Kova wakati akizungumza na mtandao huu ambapo alisisitiza kuwa anayehitajika kufika katika kituo hicho ni Gwajima na mwanasheria wake.

Kamishna Kova alisema ni vema wafuasi hao wakaendelea na kazi zao za uzalishaji,kwani kwenda kituoni hapo bila mwito au kukamatwa ni kosa.

Kova alisema eneo hilo haliruhusiwi watu kukusanyika, hivyo kwa usalama wao ni vyema wakaendelea na shughuli zao na kuliacha jeshi hilo lifanye mahojiano na Askofu huyo wakiwa huru.

"Napenda kutumia nafuasi hii kumuomba Gwajima awaambie wafuasi wake hawahitajiki kufika eneo hilo kwani anayehitajika ni yeye na mwanasheria wake," alisema Kova.

Kova alisema iwapo kila mtu atafuata taratibu hakuna nguvu itakayotumika kutoka jeshi la polisi, lakini endapo watakiuka hakuna njia mbadala ambayo inaweza kutumika zaidi ya kutumia nguvu.

Kauli ya Kova inakuja kutokana na kauli ya Gwajima aliyoitoa wakati wa sikukuu ya pasaka kuwataka wafuasi wake kujitokeza katika kituo hicho wakati atakapokwenda kuhojiwa.

Gwajima alisema lengo la kuwataka wafuasi hao kujitokeza ni ili waweze kujua kila kitu kinachoendelea katika sakata hilo kwani kuna taarifa ambazo zimekuwa zikizushwa na watu kupitia mitandao mbalimbali.

Akizungumzia hali ya usalama katika jiji la Dar, Kova alisema ni shwari na kuahidi kuwa wanaendelea na oparesheni ya kukamata wauza dawa za kulevya, wahalifu na kulinda maeneo ya fukwe.

Pia, alisema wamejipanga kukabiliana na vitendo vya kigaidi ambapo wanafanya uchunguzi kila mahali kwa kutumia vikosi vya mbwa, farasi,helkopta, magari, pikipiki na kutembea kwa miguu katika maeneo yote ya jiji.

No comments: