Mahojiano baina ya Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima na Polisi yanatarajiwa kuendelea leo katika Kituo Kikuu cha Polisi, jijini Dar es Salaam.
Mahojiano hayo yanaendelea baada ya kuahirishwa wiki iliyopita kutokana na kile kilichodaiwa kuwa afya yake ilikuwa haijaimarika vizuri na hivyo kuwalazimu polisi kuahirisha mahojiano hayo ili kumpatia muda zaidi wa kupumzika na kuendelea na matibabu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wakili anayesimamia kesi yake, John Mallya, alisema mteja wake kwa sasa afya yake imeimarika na yupo tayari kuendelea na mahojiano kesho.
“Mteja wangu anaendelea vizuri na afya yake imeimarika na yupo tayari kuendelea na mahojiano hapo kesho (leo) kama tulivyopangiwa,” alisema Mallya.
Gwajima alifikishwa polisi mwishoni mwa mwezi uliopita kwa kile kilichodaiwa kumkashifu kiongozi mwenzake wa dini na kumtolea lugha chafu. Kitendo hicho kiliwalazimu polisi kutoa mwito kwa kiongozi huyo wa dini kujisalimisha polisi ili kujibu tuhuma hizo.
Hata hivyo kiongozi huyo aliitikia mwito na kwenda kuripoti kituoni hapo ambapo alihojiwa kwa saa kadhaa na kudaiwa kuzimia wakati mahojiano yakiendelea na kukimbizwa hospitali ya TMJ kwa ajili ya matibabu.
Kiongozi huyo alilazwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) kwenye hospitali ya TMJ iliyopo Mikocheni, Dar es Salaam huku akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi ambapo baadae ilidaiwa kulikuwa na njama za kumtorosha hospitalini hapo.
Njama za kumtorosha Gwajima zilikuja kubainika na polisi na kupelekea wafuasi wake waliopanga njama hizo kukamatwa na polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Baada ya siku mbili kiongozi huyo pamoja na wafuasi wake walipatiwa dhamana katika kituo cha polisi Oysterbay na kutakiwa kuripoti polisi wakisubiri uchunguzi dhidi yao ukamilike.
No comments:
Post a Comment