Mwamvita Makamba anusurika kifo Afrika Kusini - LEKULE

Breaking

17 Apr 2015

Mwamvita Makamba anusurika kifo Afrika Kusini





Dar es Salaam. Mtoto wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Yusufu Makamba, Mwamvita Makamba amenusurika kifo nchini Afrika Kusini baada ya kundi la watu wasiojulikana kuvamia gari lake na kumrushia risasi.

Mwamvita, ambaye anafanya kazi nchini humo alikumbana na kadhia hiyo juzi usiku alipokuwa akisafiri kutoka Johannesburg kuelekea Sun City kwa shughuli za kiofisi.

Akizungumzia tukio hilo jana kutoka Afrika Kusini, Mwamvita alisema katika safari yake hiyo alifika sehemu ambayo alikuta matairi yamechomwa na kuona kundi la watu jambo lililomfanya ageuze gari haraka.

“Sehemu nyingi hapa Afrika Kusini wana vurugu sana kama Serikali haijawatekelezea mahitaji yao, hivyo katika eneo hilo ambalo nilikuta watu hao wakati napita niligundua kulikuwa na vurugu nikageuza gari,”alisema na kuongeza:

“Wale watu wakaanza kurusha mawe na wakapiga risasi ambayo ilivunja kioo cha gari langu na ilidondoka kwenye kiti cha pembeni kwenye gari. Nashukuru Mungu haikunipata. Nikaendesha hadi kituo cha polisi kutoa taarifa.”

Alisema tukio hilo halihusiani na kinachoendelea sasa katika mji wa Durban kwa Waafrika Kusini kuwakimbiza na kuua wageni bali ni jambo la kawaida nchini humo kutokea vurugu za mara kwa mara.

No comments: