Sitta ‘atimua’ vigogo TRL, amhamisha Kipande TPA - LEKULE

Breaking

17 Apr 2015

Sitta ‘atimua’ vigogo TRL, amhamisha Kipande TPA





Dar es Salaam. Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta amemsimamisha kazi kwa muda mkurugenzi mtendaji wa Kampuni ya Reli (TRL), Kipallo Kisamfu na watumishi wengine wanne baada ya ripoti ya uchunguzi kuwahusisha na sakata la ununuzi wa mabehewa mabovu 274 na kulisababishia shirika hasara ya Sh230 bilioni.

Wakati kigogo huyo wa TRA akisimamishwa, Waziri Sitta pia alitangaza kurejeshwa kazini kwa aliyekuwa akikaimu nafasi ya mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Bandari, Madeni Kipande, lakini akasema atapangiwa kazi nyingine.

Watendaji wengine wa TRL waliosimamishwa ili kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yao ni mkurugenzi mkuu wa ndani wa TRL, Jasper Kisiraga, meneja mkuu wa manunuzi, Fedinarnd Soka, mhasibu mkuu, Mbaraka Mchopa na mhandisi mkuu wa mitambo, Ngosomwile Ngosomiles.

Machi 21, mwaka juzi, TRL iliingia mkataba wa kununua mabehewa hayo aina ya Ballist Hopper Bogie (BHB) kutoka kampuni ya M/S Hindusthan Engineering and Industrial Limited ya India yenye thamani ya Sh4.316 bilioni kwa ajili ya kutumika katika uimarishaji wa njia za Reli ya Kati na yaliwasili Julai mwaka jana.

Hata hivyo, baada ya kuanza kazi yalilalamikiwa kuwa hayakuwa na ubora unaotakiwa na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe aliunda kamati kwa ajili ya kuchunguza tuhuma hizo na kamati iliyo ilikabidhi ripoti yake Desemba Mosi mwaka jana na waziri huyo kuahidi kuishughulikia bodi ya zabuni ya TRL.

Akitangaza kwa waandishi wa habari uamuzi wa kusimamisha watendaji hao jana, Sitta alisema kamati ya uchunguzi iliyoundwa imebaini kuwa wazabuni wa mabehewa hayo walilipwa fedha kinyume cha masharti ya mkataba baada ya kupewa asilimia 100 ya malipo.

“Inaonekana kuwa mazingira ya utekelezaji wa mkataba huu yana dalili za hujuma kwa TRL na kwa nchi yetu na siyo uzembe tu,” alisema Sitta.

“Tutaunda kamati ya kuchunguza tuhuma zao, itakayojumuisha ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali(AG), Takukuru na Ofisi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi katika sekta ya Umma(PPRA),” alisema Sitta.

Sitta alisema kamati hiyo itafanya kazi ndani ya wiki tatu kuanzia Jumatatu ya Aprili 20 na kwamba taarifa ya kamati hiyo itatoa mwelekeo na ushauri wa hatua gani zifanyike ili kukomboa fedha zilizopotea wakati wa malipo ya mabehewa hao.

“Wakati naingia wizarani nilikuta tayari mabehewa 150 yameshaingia yakiwa mabovu hivyo, hivyo kwa hivyo ikanibidi kusitisha kwanza yale mengine 124 yasiletwe,” alisema Sitta.

“Kilichonishtua zaidi ni baada ya kupitia mchakato wa malipo ya mabehewa hayo na kukuta walishalipwa asilimia 100 yote ikiwa ni kinyume cha mkataba, uliotaka kulipa asilimia 50 kwanza, baada ya kumaliza kuyaingiza asilimia 40 nyingine walipwe na baada ya kufanya kazi mwaka mmoja ndio walipwe asilimia 10 iliyobakia lakini haikuonekana hatua hiyo.”

Kutokana na hatua hiyo, Sitta aliagiza Bodi ya Wakurugenzi wa TRL kufanya kikao cha dharura kuteua watumishi wenye sifa za kukaimu nafasi hizo mpaka uchunguzi utakapokamilika.

Kuhusu kurejeshwa kazini kwa Kipande, taarifa ya Wizara ya Uchukuzi imeeleza kuwa kigogo huyo hatarejeshwa kazini kuendelea kukaimu nafasi ya ukuu wa bandari kwa kuwa uongozi wake ulikuwa unalalamikiwa na wateja na wadau wa bandari.

“Baada ya kuisoma taarifa ya Tume na hatimaye kushauriana na taasisi mbalimbali zinazohusika na masuala haya, tumeridhika pasipo shaka yoyote kwamba isingefaa Ndugu Madeni Kipande kuendelea na kazi ya kuongoza Mamlaka ya Bandari,” inasema taarifa hiyo.

“Kutokana na hali hiyo, Serikali imeamua kumrejesha Ndugu Madeni Kipande Idara Kuu ya Utumishi ili aweze kupangiwa majukumu mengine,” inasema taarifa hiyo ambayo imeongeza kuwa Awadhi Massawe ataendelea kukaimu nafasi ya mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo nyeti kwa uchumi wa nchi.

Katika hatua nyingine, Sitta alizungumzia changamoto ya usafiri wa treni jijini Dar es Salaam akisema kikwazo kikubwa katika usafiri huo ni kutumika kwa mashine ziilizochakaa.

Sitta alisema kwa sasa wizara yake imeshaagiza vichwa vya treni vinne kutoka karakana ya Morogoro ambavyo vitaletwa Dar es Salaam kwa ajili ya safari za treni hizo zilizopachikwa jina la “Treni za Mwakyembe”.

“Pamoja na hatua hiyo pia kuna mazungumzo ambayo tumeshafanya na kampuni ya Kifaransa ambayo itakuja Tanzania wakati wowote kufanya uchunguzi wa miundombinu na kuangalia jinsi gani tunaweza kuwekeza katika usafiri wa treni hapa jiji la Dar es Salaam. Kampuni hiyo inaitwa Alstorm ambayo itafanya kazi hiyo miezi sita,” alisema Sitta.

“Lengo la kufanya hivyo ni kutaka kuangalia kama miaka ijayo tunaweza kuanzisha usafiri wa treni kwenda Mbagala, Gongo la Mboto, Temeke na Maeneo mengine ya mbali hapa jijini.”

Kuhusu Viongozi wa dini

Katika hatua nyingine, Sitta ametetea mpango wa Serikali kuzifungia taasisi na vyama vinavyojihusha na harakati za kuchochea makundi ya kijamii kupinga Katiba inayopendekezwa.

Juzi, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe alisema Serikali itaanza kufanya ukaguzi wa vyama na taasisi hizo ili kujiridhisha na usajili wake na kutoa tahadhari kwa taasisi hizo kujihusisha na siasa.

Akizungumza katika mahojiano na Mwananchi, Sitta ambaye alikuwa mwenyekiti wa Bunge la Katiba, alisema: “Itakuwa ni jambo la kushangaza sana kwa viongozi wa dini kuonekana wakishinikiza waumini wao kutopigia kura ya ndiyo Katiba inayopendekezwa. Kama ni hivyo basi tusingekuwa na vyama vya siasa.”

No comments: