Moyo aibua mjadala mzito Z’bar - LEKULE

Breaking

21 Apr 2015

Moyo aibua mjadala mzito Z’bar


Zanzibar. Wanasiasa wa Zanzibar wamegawanyika kuhusu hatua ya CCM kumfukuza uanachama mwanasiasa mkongwe, Hassan Nassor Moyo (pichani) baada ya kupatikana na hatia ya kuvunja miiko na maadili ya chama kwa kitendo chake cha kuhudhuria mikutano ya hadhara ya CUF na kutetea mfumo wa muundo wa Serikali tatu kinyume na sera ya chama chake.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti siku moja baada ya mwanasiasa huyo kufukuzwa, baadhi ya wanasiasa walisema kuwa CCM imefanya kosa kwa kutompa nafasi ya kujitetea juu ya tuhuma zilizokuwa zinamkabili.

Aliyekuwa Kamishina wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Muhamad Yussuf Mshamba alisema kama Moyo alikuwa na makosa, alitakiwa kuitwa kwenye vikao vya chama kuhojiwa kuhusu tuhuma zilizokuwa zinamkabili katika ngazi zote badala ya kumtimua kibabe.

Alisema utaratibu uliotumika kumfukuza ni kinyume na Katiba ya CCM pamoja na misingi ya demokrasia kwa vile amehukumiwa bila ya kupewa nafasi ya kujitetea kwenye vikao ili kuhakikisha haki inatendeka kabla ya kufanyika uamuzi.

“Mwanachama anapovunja miiko, maadili au kanuni za chama uchunguzi peke yake hautoshi kutoa adhabu. Moyo alitakiwa kuitwa na kujitetea kama kweli alifanya makosa kabla ya kufukuzwa,” alisema Mshamba ambaye pia mwanadiplomasia mstaafu.

Naibu Katibu Mkuu wa ADC Zanzibar, Ali Makame Issa alisema mambo yaliyomkuta Moyo ni ya kujitakia kwa sababu kila chama kimeweka miiko, maadili na kanuni, hivyo mwanachama anapokwenda kinyume lazima achukuliwe hatua.

“Vyama vya siasa vina utaratibu wake ukienda nje ya utaratibu utapewa adhabu tu. Moyo alifika pahala unashindwa kumfahamu kama ni CUF au CCM anatofautiana hadi na sera za chama chake,” alisema Ali.

Alisema pamoja na CCM kuwa na wasemaji wake, lakini Moyo alijigeuza msemaji wa CCM na kupinga misingi ya Mapinduzi na Muungano wa Tanganyika bila ya kujali sera ya chama chake.

Kuhusu kupewa nafasi ya kujitetea, Katibu wa CCM Mkoa wa Mjini Magharibi, Aziza Mapuri alisema walikuwa wakimwandikia barua za wito kwa ajili ya kuhojiwa na vikao kuanzia ngazi ya wilaya hadi mkoa, lakini Moyo alikuwa akipiga chenga kuhudhuria.

“Kikao cha mwisho cha mkoa tulimwita kwa kumuandikia barua kabla ya kumjadili na kumfukuza lakini baadaye alitupigia simu na kutuambia yeye ni mtu mzima hawezi kuhangaika na kutaka kikao kikafanyike nyumbani kwake lakini mikutano ya CUF na makongamano anaudhuria Unguja na Pemba,” alisema Mapuri.

Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Mjini Unguja, Baraka Shamte alisema Moyo amejichinja na kisu chake mwenyewe kwa sababu alikuwa anafahamu vizuri kanuni, miiko na maadili ya chama chake kwa sababu alishiriki kuzitunga baada ya kuzaliwa kwa CCM Februari 5, 1977.

“Moyo ameshiriki kutunga Katiba na kanuni za chama lakini ameshindwa kuheshimu miiko na maadili na kuamua kujichinja na kisu chake mwenye,” alisema.

Mkurugenzi wa Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salim Bimani alisema kitendo cha CCM kumfukuza Moyo kinaonyesha jinsi kilivyopoteza mwelekeo kwa kukosa viongozi bora. Alieleza kushangazwa kwake na hatua hiyo ya kumfukuza Moyo licha ya mchango wake mkubwa katika harakati za ukombozi wa Zanzibar.

Bimani alisema kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kila Mtanzania ana haki ya kutoa maoni yake na hatua ya kumfukuza kutokana na kutofautiana kimtazamo kuhusu mfumo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, haikuwa mwafaka katika misingi ya utawala bora.

Moyo ajibu

Akizungumzia kutimuliwa kwake, Moyo alisema ataendelea kutetea mfumo wa Muungano wa Serikali tatu hadi Zanzibar itakapofanikiwa kupata mamlaka kamili ya kujitawala na kujiamulia mambo yake kama ilivyokuwa kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964 licha ya kufukuzwa CCM juzi.

No comments: