Wanasiasa wabuni mbinu ya ‘kuchota’ wapiga kura - LEKULE

Breaking

21 Apr 2015

Wanasiasa wabuni mbinu ya ‘kuchota’ wapiga kura


Dar es Salaam. Kuna kila dalili kuwa wanasiasa nchini wamebuni mbinu mpya ya kuzitumia klabu za mbio za pole maarufu kama ‘jogging’ kutekeleza mikakati ya kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu, mwaka huu.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa na baadhi ya wananchi waliliambia gazeti hili kwa nyakati tofauti jana kuwa matukio ya kijamii yanayoendelea hivi sasa nchini na kuhusisha wanasiasa yanapaswa kutazamwa kwa jicho la karibu.

Juzi kulikuwa na matukio makubwa mawili katika maeneo tofauti jijini hapa yaliyohusisha matembezi ya kilomita kadhaa yaliyokuwa yakifanya kampeni mbili tofauti na kuhusisha vigogo wa ngazi ya juu wa CCM.

Katika tukio la kwanza, vijana wapatao 10,000 kutoka klabu mbalimbali za mbio za pole wakiongozwa na wenyeji wao Temeke Family, walimwalika Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa kuongoza matembezi ya kulaani na kupinga ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino).

Lowassa katika tukio hilo aliambatana na wabunge Idd Azzan (Kinondoni), Mussa Zungu (Ilala) na Abbas Mtemvu (Temeke) aliyekuwa mwenyeji wa matembezi hayo yaliyoanzia Uwanja wa Taifa hadi Viwanja vya TCC Chang’ombe.

Katika upande mwingine, jimboni Segerea, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akiongozana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye waliongoza klabu 100 za ‘jogging’ kuhamasisha vijana wajiandikishe katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Wakati wa kuanza hotuba yake, Lowassa alisema hawezi kuzungumza kwa kirefu kutokana na kifungo kinachomkabili cha kutumikia adhabu ya kuanza kampeni za urais mapema alichopewa na chama chake.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda alisema kipindi kama hiki wanasiasa hutumia kila mbinu ya kuongeza ushawishi kwa wapiga kura, hivyo matumizi ya klabu za mbio za pole ni moja ya njia za kukuza umaarufu wao.

“Kitendo cha mwanasiasa kushiriki kwenye klabu za ‘jogging’ kinatengeneza ngome ya umaarufu, ataonekana na kuandikwa kwenye vyombo vya habari. Siasa ni vita. Wapo wengine wanatumia hadi njia za kuandika vitabu ili jamii iwakubali,” alisema Mbunda.

Alisema matukio yoyote yanayoendelea na kuhusisha wanasiasa yasipuuzwe licha ya mengine kugusa masuala ya kijamii ambayo ni vigumu mtu kuyang’amua kuwa yanahusisha siasa.

Mkazi wa Chang’ombe, Hamis Juma aliyekuwapo katika matembezi ya Lowassa, alisema utaratibu wa kutumia klabu hizo kuhamasisha masuala mbalimbali ya kijamii ni mzuri ila unaonekana kupata umaarufu sasa kutokana na kuwa na manufaa kwa wanasiasa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ujao.

Hata hivyo, Nape jana aling’aka na kusema ifikie kipindi jamii iache itikadi za kisiasa katika masuala ya msingi kwa maendeleo ya Taifa.

Mwenyekiti wa kllabu ya mbio za pole ya Temeke Family, Hassan Muharami alisema lengo la kampeni hizo ni kulaani na kupinga mauaji ya albino yanayoendelea nchini na siyo siasa.

Alisema kilabu yao huwakusanya vijana kutoka manispaa zote za Mkoa wa Dar es Salaam ili washiriki katika michezo na masuala ya jamii.

No comments: