Dar es Salaam. Kamati Kuu ya Chama cha Tanzania Labour (TLP), imempendekeza Mwenyekiti wa chama hicho, Augustine Mrema kutetea kiti chake cha ubunge katika jimbo la Vunjo.
Kaimu Katibu Mkuu wa TLP Nancy Mrikaria, aliliambia gazeti hili jana kuwa kamati hiyo pia imemthibitisha Mrema kuendelea na nafasi yake ya uenyekiti wa chama hicho kwa kipindi kingine.
Alisema kamati imeridhia Mrema kuendelea kugombea ubunge katika jumbo la Vunjo ikiwa na imani kuwa ana nafasi kubwa ya kushinda, ikilinganishwa na wengine watakaojitokeza kupambana nao.
“Kamati imefikia hatua hiyo kwa kutambua uwezo alionao mwenyekiti katika kukiendeleza chama, pia hadi sasa hakuna mwanachama mwingine aliyejitokeza kugombea nafasi hiyo na tulianza kutoa fomu tangu Aprili 9 hadi 17, wakati kwenye nafasi ya makamu mwenyekiti Bara ndiyo kuna ushindani wa watu wawili wanaoigombea,” alisema Mrikaria
Alisema nafasi ya Makamu Mwenyekiti upande wa Zanzibar pia haina mpinzani kwa kuwa hadi sasa aliyechukua fomu ni Alhaji Hamad Mkadam ambaye ndiyo anashika nafasi hiyo.
“ Tunatarajia wajumbe wa mkutano watajitokeza kwa wingi ili kufanikisha uchaguzi huo ambao ni muhimu kwa maendeleo ya chama, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu kwa kuwa ukikamilika tunapata nafasi ya kujipanga,” alisema Mrikaria.
Naye Mrema alisema kwamba anaamini kwamba kamati hiyo imempendekeza kutokana na kuwa na imani naye kwamba ana uwezo mzuri wa kukiendeleza chama hicho.
“ Siyo kwamba nitakuwa nagombea kwa ubabe au ujeuri bali kamati yenyewe imenibariki, naamini Vunjo nitashinda na kuendelea kukifanya chama kistawi kwani nisipokitetea chama kitakuwa kama cha wacheza ngoma,” alisema Mrema.
Hadi kufikia hatua hiyo ya kufanya uchaguzi TLP ilibanwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, kwa kupewa siku 80 kwa uongozi kuhakikisha kinafanya uchaguzi wake wa ndani ili kuwapata viongozi wapya.
Msajili alitoa siku hizo baada ya baadhi ya wanachama wa chama hicho kufikisha malalamiko wakiiomba itangaze kwamba uongozi wa Mwenyekiti Mrema unakiuka katiba ya chama hicho, wakidai anakiongoza kidikteta hivyo kuporomosha heshima ya chama.Akizungumza ofisini kwake, Dar es Salaam jana, Msaidizi wa Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza alisema baada ya kusikiliza pande zote zinazosigana, ofisi hiyo iliwataka viongozi kuandaa uchaguzi na tayari wameshapeleka barua ya ratiba ya uchaguzi huo.
No comments:
Post a Comment