Arusha. Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kumpa nishani ya Taifa, mgunduzi wa madini ya Tanzanite, Jumanne Ngoma aliyeyagundua miaka 48 iliyopita.
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene alisema hayo jana katika maonyesho ya nne ya kimataifa ya madini ya vito yanayoendelea mjini hapa.
Waziri Simbachawene alisema Serikali imetambua ubunifu wa Ngoma na hakuna shaka ndiye mgunduzi sahihi wa madini hayo yanayochimbwa Mererani wilayani Simanjiro.
“Mzee Ngoma Rais amekubali ugunduzi wako na atakupa nishani yake ya Taifa ya kutambua na kuthamini mchango wako,” alisema.
Mara baada ya taarifa hiyo, Ngoma aliishukuru Serikali kwa kutambua ugunduzi wake.
“Tuendapo tutanufaika sana kutokana na ugunduzi wangu wa madini ya Tanzanite ambayo ni ghali duniani,” alisema Ngoma.
Baadhi ya wafanyabiashara wa madini, wakiwamo wakurugenzi wenza wa Kampuni ya Tanzanite One, Faisal Juma na Hussein Gonga, walisema Serikali imefanya vyema kutambua umuhimu wa Ngoma.
No comments:
Post a Comment