Rungwe. Wakazi wa Kijiji cha Ikama wilayani Rungwe wameilalamikia Kampuni ya Tanzania Oxgyen Ltd (TOL), inayochimba gesi asilia katika eneo kwa kushindwa kuchangia huduma za jamii kwa wananchi.
Meneja wa kampuni hiyo, Benard Matiku alikiri kuwapo kwa changamoto hiyo, akisema kwamba suala hilo liko mikononi mwa mmiliki.
Mkazi wa kijiji hicho, Sunday Hassan alisema tangu mwekezaji huyo aanze kuvuna gesi mwaka 2012, hakuna ahadi iliyotekelezwa na wananchi wanazidi kutilia shaka uwapo wa mwekezaji huyo.
Hassan alisema kijiji kilimtaka mwekezaji ajenge zahanati, barabara na vyumba vya madarasa, lakini hajachangia chochote.
Mkazi mwingine, Janken Mwangomango alisema pia vijana wa eneo hilo hawajapewa ajira ili kujikomboa na umaskini.
Luciana Desa alisema hata wanawake wanaendelea kutumia kuni badala ya gesi licha ya kuwapo kwa kampuni hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Zainabu Mbuse alisema malalamiko ya wanakijiji hao aliyapata Aprili 8, mwaka huu alipotembelea eneo hilo.
Alisema atalifanyia kazi ili wananchi wafaidike na gesi hiyo.
No comments:
Post a Comment