Mpigania ukombozi wa Afrika Brig Jen Mbita afariki dunia - LEKULE

Breaking

27 Apr 2015

Mpigania ukombozi wa Afrika Brig Jen Mbita afariki dunia


Dar es Salaam. Katibu mtendaji wa iliyokuwa Kamati ya Ukombozi Kusini mwa Afrika, Brigedia Jenerali Hashim Mbita (82), amefariki dunia jana saa tatu asubuhi katika Hospitali ya Jeshi, Lugalo, Dar es Salaam.

Mbita amekuwa akisumbuliwa na maradhi ya moyo katika kipindi cha miezi minane iliyopita.

Mtoto wa marehemu, Iddi Mbita alisema jana nyumbani kwa marehemu Chang’ombe, Dar es Salaam kuwa afya ya baba yake imekuwa ikibadilika mara kwa mara.

Alisema siku tatu zilizopita, hali yake ilikuwa mbaya kiasi cha kulazimika kuwekewa mipira ya kumsaidia kula.

“Jana mzee aliamka vizuri asubuhi, lakini muda mfupi baadaye hali yake ikabadilika na kufariki dunia,” alisema.

Kuhusu mazishi, alisema yatafanyika keshokutwa saa 10 alasiri katika Makaburi ya Kisutu baada ibada ya kumuaga kwenye Msikiti wa Mtoro, Kariakoo.

“Msiba utakuwa hapahapa nyumbani kwake, Chang’ombe. Upande wa familia tutakuwa na taratibu zetu, lakini upande wa Serikali na jeshi pia watakuwa na utaratibu wao wa mazishi,” alisema.

Rais Kikwete atuma salamu

Rais Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu kutokana na kifo hicho.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu iliiagiza Serikali na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kushirikiana na familia katika kuandaa mazishi hadi maziko ya kiongozi huyo.

Balozi Tambwe amwelezea

Akimzungumzia marehemu Mbita, aliyekuwa mbunge wa Tabora Mjini, Balozi Saleh Tambwe alisema Watanzania wanamfahamu Mbita, lakini nchi alizozipigania hadi kupata uhuru ndizo zinazomfahamu zaidi.

Alisema Mbita ndiye kiongozi wa kwanza wa Kamati ya Ukombozi Kusini mwa Afrika kwenda kwenye mapambano.

Alisema viongozi wengine waliomtangulia walikuwa ni raia wa kawaida na hawakuwahi kwenda vitani.

“Unapomzungumzia Mbita, nchi za Msumbiji, Angola, Zimbabwe, Namibia na Afrika Kusini ndizo zinazomfahamu vizuri.

“Wao ndiyo wanaweza wakauzungumzia ujasiri wake na jinsi alivyowaongoza katika mapambano dhidi ya wakoloni,” alisema Tambwe ambaye aliwahi kuwa Balozi wa Rwanda, Zambia na Uganda kati ya 1977 – 2004.

Balozi Tambwe aliongeza kuwa miaka iliyopita, Rais Mstaafu wa Msumbiji, Joachim Chisano aliwahi kwenda Tabora kumtembelea Mbita na alikaa katika nyumba yake wakati wote wa likizo akiwa Tanzania.

“Nimemfahamu Mbita nikiwa Balozi wa Zambia, yeye akiwa ni Katibu Mtendaji wa Kamati ya Ukombozi iliyokuwa na Makao yake makuu nchini humo.

Kulazwa

Septemba mwaka jana, Brigedia Mbita aliwahi kulazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, kitengo cha moyo kabla ya kuhamishiwa chumba cha uangalizi maalumu katika hospitali hiyo baada ya hali yake kubadilika.

No comments: