Treni ya kisasa yazinduliwa Dar es Salaam - LEKULE

Breaking

26 Mar 2015

Treni ya kisasa yazinduliwa Dar es Salaam

Raisi wa Burundi Pierre Nkurunzinza akipeperusha bendera kuashiria kuanza kwa safari za treni ya kisasa katika kituo cha Reli cha Dar es salaam jana huku Raisi Jakaya kikwete  na viongozi wengine wa nchi za Afrika mashariki wakishuhudia.
TRENI nne za kisasa za mizigo mali ya Shirika la Reli nchini (TRL) zinazokwenda nchi nne za Ukanda wa Kati zimezinduliwa jana jioni Dar es Salaam kwenda kwenye nchi hizo, tukio lililoshuhudiwa na marais na wawakilishi wa nchi husika.
Nchi hizo ni Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Rwanda na Uganda ambapo mwenyeji wao Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete aliongozana nao kuzindua treni hizo, ikiwa ni moja ya mikakati ya kuendeleza Ukanda wa Kati.
Uzinduzi wa treni hizo, ulitanguliwa na mkutano wa marais hao waliokutana jana jijini Dar es Salaam, kuzungumzia masuala mbalimbali ya uwekezaji kwenye ukanda huo.
Mkutano huo unaendelea leo, ambapo marais hao watazungumza na wawekezaji mbalimbali. Marais waliokutana ni pamoja na mwenyeji wao Rais Jakaya Kikwete, Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Pierre Nkurunziza wa Burundi, Kenya iliwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Amina Muhammed na Rwanda iliwakilishwa na Waziri wa Miundombinu, James Musoni na DRC iliwakilishwa na Waziri wa Miundombinu, Justine Mwanangongo.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano wa marais hao, uliohudhuriwa pia na baadhi ya mawaziri, Rais Kikwete alisema mradi mwingine wa ujenzi wa reli mpya ya Ukanda wa Kati inayoanzia Dar es Salaam hadi Msongati utaanza kujengwa Juni mwaka huu.
Ujenzi wa mradi huo utakamilika baada ya miaka minne, na lengo lake ni kuendelea kuziunganisha nchi za ukanda huo ili ziweze kukua zaidi kiuchumi na kuwa na tija kwa maendeleo yao.
Rais Kikwete alisema reli hiyo ni muhimu kwani ni kiungo kati ya nchi hizo na kwamba ujenzi wake unaanzia Dar es Salaam-Isaka-Kigali- Kitega/Keza hadi Msongati na unatekelezwa na mkandarasi M/s CANARAIL/GIBB Africa.
Alisema ujenzi huo utakapokamilika, utakuwa kiungo muhimu na bora kwa usafirishaji wa mizigo inayotoka bandari ya Dar es Salaam kwenye nchi hizo na kwamba utapunguza gharama za usafiri kwa njia ya barabara.
“Huu ni mradi mkubwa, ukianza utafungua uwekezaji kwenye ukanda wetu huu wa Kati, lakini tunafanya uchunguzi ili kuona uwezekano wa ujenzi wa reli nyingine ya Isaka, Mwanza, Tabora, Kigoma, Uvinza, Msongati, Kitega na Kaliua kwenda Mpanda”, alisema Rais Kikwete.
Alisema mradi wa ujenzi wa reli hiyo mpya ya kisasa, hautaua reli ya awali ya Kati, kwani nayo iko kwenye hatua za ukarabati kwa kuimarisha ubora na kuifanya reli hiyo iwe ya kisasa zaidi.
Akizungumza jinsi ya kuimarisha Ukanda huo, Rais Kikwete alisema ni lazima nchi hizo ziweze kuzalisha umeme wa kutosha na kwa bei nafuu, kwani rasilimali za kuzalisha umeme huo zipo.
“Tuna rasilimali za kutosha kuzalisha umeme utakaokidhi mahitaji kwa nchi zetu, kikubwa ni nidhamu ya kusimamia ndio itakayotufanya Ukanda huu kuwa na umeme wa kutosha na hata wa ziada tutakaoweza kuzalisha na kuuza nje, ila cha ajabu nchi zetu zote kwa sasa hazina umeme wa kutosha,” alisema Rais Kikwete.
Akimwakilisha Rais wa Rwanda, Paul Kagame, Waziri wa Miundombinu, James Musoni alisema maoni ya Rais Kagame ni kuona maendeleo ya kiuchumi katika Ukanda wa Kati na kwamba mkutano huo unaongeza nguvu na utulivu katika ushirikiano.
Alisema mashauriano ya mara kwa mara katika ngazi ya wakuu wa nchi yanasaidia kuharakisha na kuongeza juhudi za kujiletea maendeleo na kwamba, Rwanda ipokushirikiana na washirika wengine katika Ukanda wa Kati.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Amina Mohammed (pichani) aliyemwakilisha Rais Uhuru Kenyatta, alisema Kenya inashiriki kuonesha mshikamano wa agenda ya jukwaa la mkutano wa Wakuu wa Nchi katika Ukanda wa Kati na wawekezaji na kumpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa mpangilio mzuri wa mkutano.
Waziri Mohammed alisema suala la sekta ya usafirishaji ni muhimu kwa maslahi ya nchi za ukanda huo na kwamba mkutano huo utawezesha kubaini mianya iliyopo katika sekta hiyo na ambayo inahitaji kuzibwa kwa manufaa na faida ya wananchi wa nchi hizo.
Alibainisha pia gharama za usafiri ni kubwa kati ya asilimia 30 na 40 na kwamba kuna haja ya wadau kujadiliana na kurekebisha mapungufu hayo na kuahidi kuwa Kenya itaendelea kusaidia uboreshaji wa sekta ya usafiri kwa manufaa kibiashara na kuvutia wawekezaji zaidi katika Ukanda huo wa Kati.

No comments: