Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema kuwazuia
wananchi kwenda nyumbani kwake kumshawishi agombee urais katika Uchaguzi
Mkuu wa Oktoba mwaka huu ni sawa na kuzuia mafuriko kwa mkono.
Lowassa
alitoa kauli hiyo nyumbani kwake mjini Dodoma jana wakati
alipotembelewa na kundi jipya kutoka Mbarali mkoani Mbeya waliokwenda
kumshawishi atangaze nia kugombea urais.
Lowassa ametoa
kauli hiyo siku moja baada ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape
Nnauye kusema kuwa kwa kuandaa makundi ya kumshawishi, mbunge huyo wa
Monduli anajua adhabu yake na anaweza kupoteza sifa za kuwa mgombea
urais kupitia CCM.
“Sasa mmekuja siku mbaya kwa sababu
jana kuna watu wamesema maneno mengi mabaya ambayo kwa malezi yangu mimi
mambo ya chama humalizwa kwenye vikao vya chama na siyo kwenye vyombo
vya habari. Mnazungumza, mnaelewana mnatoka pale,” alisema.
“Na
utaratibu huu ulioanzishwa na watu, mimi ni vigumu kuuzuia, utazuiaje
mafuriko kwa mikono? Mafuriko yanakuja halafu nazuia kwa mikono nitaweza
kweli? Hawa watu sina hoja nao, sina cha kuwaambia,” alisema.
Mambo ya chama
Lowassa
ambaye hivi karibuni aliweka bayana kuwa ameshawishika kuwania nafasi
hiyo, alisema, “Lakini mambo ya chama hayawezi kuwa kwenye ma-TV,
magazeti na maredio, mara huyu hivi, mara huyu vipi. Mkiona chama
kinakwenda kwa utaratibu huo, ni hatari sana, CCM ninayoijua mimi ni ya
vikao.”
Alisema hakusudii kujibu hizo hoja (za Nape) bali rafiki yake Hussein Bashe amezielezea vizuri.
“Niseme
mawili tu yanayonisikitisha wanasema eti nawaiteni, nakupeni fedha,
mimi hela natoa wapi? Lakini kibaya zaidi nikiweka maturubai hapa ni
kosa, mkiwa na viti hapa ni makosa? Na wanasema nawapeni chakula mambo
ya ajabu sana na yanasemwa na watu wazima wenye heshima
zao,” alisema Lowassa na kuongeza:
“Juzi
walikuwapo vijana 300 hapa, nitawapikia chakula nitawaweza? Nyie kwa
wingi huu mtaenea hapa? Lakini ni vibaya unamdhalilisha binadamu
mwenzako kuwa maisha yake yote ni kufikiria tumbo. Hamna cha kufikiri
isipokuwa tumbo, kwa hiyo mnakuja hapa kwa sababu mnataka Lowassa
awapeni chakula, ni kudhalilisha watu.”
Alisema watu
wanaofika nyumbani kwake wanafanya hivyo kwa utashi, hiari na gharama
zao wenyewe na wengine yeye hawafahamu kabisa.
Lowassa alisema hajawahi kuwaona, wala kuwatuma kufanya
hivyo au kuwaomba kufika nyumbani kwake watu ambao wanamshawishi
kutangaza nia ya kugombea urais.
Ushauri wa Kikwete
Aliwashauri wengine ambao hawajafika wasubiri chama kiseme nini kifanyike kwa watu wanaotaka kuja kunishawishi.
“Kwa
sababu Rais (Jakaya Kikwete), alivyokuwa Songea kule na mimi nilikuwapo
kule akasema mkiona hawa hawatoshi muda upo bado washawishini wengine
waingie, sasa mkifanya hivi ni kosa, ni kampeni.
Ipi si kampeni sasa? “alihoji Lowassa na kuongeza:
“Nawashauri
tusiingize mgogoro kwenye chama tungoje tupate maelekezo, mimi nina
uhakika kuwa tutapata nafasi. Hakika ipo siku Watanzania watapata uhuru
wa kusema juu ya mtu mimi. Watapiga kura zao kusema naam ama hapana. Kwa
hiyo tungojee siku. Nami nina hakika wako Watanzania wengi
wanaonipenda.”
Lowassa alisema, “Kwa hiyo huyo
anayepiga kelele nyingi sijui tutoke chama, sijui tufanye nini? Angojee
wanachama wa CCM na wananchi waamue. Mimi ni mwanademokrasia, ninaamini
kwenye demokrasia lakini pia kwenye utendaji bora.”
Lowassa,
ambaye bado anatumikia kifungo cha mwaka mmoja kutoka chama chake
aliwataka watu hao kujiandikisha kwa wingi na kupiga kura kwa mtu ambaye
wanaamini ataweza kuwaongoza kwa kutoa maamuzi magumu na makubwa kwa
faida ya nchi.
Juzi, Nape alisema kitendo cha makundi
ya watu kwenda kumshawishi Lowassa atangaze nia ya kuwania urais ni
kinyume cha Katiba ya CCM.
Alisema kitendo hicho ni
kampeni ya wazi ya urais anazoendelea nazo kabla ya muda kufika na
kuonya kama ataendelea atapoteza sifa za
kugombea nafasi ya urais.
Katika
kipindi cha wiki mbili sasa kwenye makazi yake Monduli mkoani Arusha na
Area C mjini Dodoma makundi ya watu mbalimbali yamekuwa yakifika
kumshawishi agombee urais baadaye mwaka huu.
No comments:
Post a Comment