Kwa nini rais ajaye awe mwanamke - LEKULE

Breaking

26 Mar 2015

Kwa nini rais ajaye awe mwanamke

Wanaharakati nchini wamesema rais ajaye anaweza kuwa mwanamke kutokana na sababu kadhaa, ikiwamo wingi na hamasa waliyonayo wanawake katika upigaji kura.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema ingawa wanatambua uchaguzi ni mapambano, wanaamini kama wanawake na jamii itakubali mabadiliko, nchi itaongozwa na rais mwanamke.
Wanaharakati hao kutoka vyama vya Umoja wa Wanawake Wanasiasa (Ulingo), Mtandao wa Jinsia Tanzania, (TGNP), Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) walisema hakuna kinachoshindikana kama wanawake wataamua.
Ulingo
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wanasiasa Tanzania (Ulingo), Anna Abdallah alisema, baada ya wanawake kuangaliwa kama kundi duni katika nyanja za siasa kwa muda mrefu, sasa ni zamu yao kujitokeza wagombee nafasi mbalimbali za uongozi, ikiwamo ya urais.
“Lengo letu sisi ni mwanamke kujitokeza, akijitokeza tutamuunga mkono kwa umoja wetu bila kujali anatoka chama gani cha siasa,” alisema mwenyekiti huyo aliyeeleza kuwa jamii ya sasa ina imani kubwa na mwanamke.
Aliongoza “Iwapo wanawake watafanya kile tunachotaka , kwa maana ya kuwaunga mkono wagombea, kupiga kura, wakati wa kupata rais mwanamke umefika. Hilo halina ubishi na linawezekana.” Anna alitaja sababu nyingine za kuwashawishi wanawake wajitokeze kugombea urais kuwa ni kuongezeka kwa uelewa wa wanawake katika masuala ya siasa.
TGNP
Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania, (TGNP), Lilian Liundi alisema wanawake kuwa viongozi siyo ajabu kwani tayari wameshafanya hivyo katika nafasi mbalimbali. Isipokuwa wanahitaji kuungwa mkono katika nafasi za kisiasa.
Alisema mtandao huo utamuunga mkono mwanamke yeyote atakayeonyesha nia ya kugombea bila kuangalia itikadi ya chama anachotoka, huku ukiamini kuwa wanawake wanaweza kufanya vizuri zaidi wanapopata nafasi.
“Japokuwa historia inaonyesha wanafanya vizuri, tunahitaji kuwaunga mkono kwa nia thabiti ili wakalete mabadiliko ya kweli, ” alisema Liundi.
 
 
Kigoda cha Taaluma
Mwenyekiti wa Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Penina Mlama, alisema kuwa huko nyuma ilikuwa kazi wanawake kuwa viongozi, lakini sasa njia ipo, kwani wapo waliotangulia kuwa viongozi na wakafanya vizuri.
Alisema moja ya mambo yatakayofanikisha hilo ni wanawake wenyewe kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika uchaguzi huo kwenye ngazi zote; udiwani, ubunge na urais.
“Wakati wa kusubiri kutengewa viti maalumu umekwisha na wanawake walitambue hilo, hivyo wajitokeze katika harakati za kugombea uongozi badala ya kusubiri kuteuliwa,” alisema na kubainisha kuwa zaidi ya asilimia 50 ya wapiga kura wa Tanzania ni wanawake.
“Kuna viongozi wanaume hawana uwezo kabisa historia inaonyesha na wanatuongoza, wamepenya katika uongozi kwa sababu wanaungana mkono na wanatafuta ushawishi, sasa kama wapo wanawake wenye uwezo wa kuongoza kwa nini wasifanye hivyo na kwa nini wasiungwe mkono kwanza na wanawake wenzao halafu wanaume wafuatie,” alihoji Profesa Mlama.
LHCR
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Bisimba alisema, kuna wanawake wamefanikiwa kupitia harakati hizi za kuwataka wagombee nafasi mbalimbali za uongozi, kwa sababu walikuwa na uwezo lakini walikuwa wagumu kujitokeza.
Alisema iwapo ushawishi kwa wanawake utapamba moto kama ilivyo sasa na wengi wakajitokeza kugombea, matokeo ya uchaguzi mkuu ujao yatashuhudia wanawake wengi wakishika nafasi mbalimbali za uongozi.
“Kuna nafasi kubwa ya kupata rais mwanamke kwa sababu wagombea wengi wanaoshinda nafasi za juu ikiwamo urais wanawategemea wanawake kama wapiga kura wao wakuu, hivyo wakijipigia wenyewe nafasi ya kushinda itakuwa kubwa, ” alisema Bisimba.
Alifafanua kuwa juhudi zao za kuwaunga mkono siyo za fedha bali kuwapa moyo na kuwajengea uwezo kwani mfumo uliopo una vikwazo vingi kwa mwanamke.
“Tunawajengea kujiamini, kusimama mbele za watu na kujinadi kwa mifano iliyo hai siyo hadithi, kuzungumza bila woga mbele za watu, tuna imani tutashinda mapambano haya,” alisema Bisimba.

No comments: