Wakati Taifa likielekea katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa
kufanyika Oktoba, mwaka huu, ushindani wa wazi wa kisiasa kati ya chama
tawala (CCM) na vyama vya upinzani kupitia Ukawa unaonekana bayana.
Kambi hizo mbili, zinatunishiana misuli huku kila moja ikijigamba kuibuka na ushindi na hatimaye kushika dola.
Licha ya kauli za majigambo kutoka kambi hizo,
bado hakujawa na uhakika kambi ipi itakamata dola. Hata hivyo, masuala
kadhaa yanatajwa kuwa vigezo vya ushindi kwa kila kambi.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema mambo
yanayotazamwa ni pamoja na uimara wa kila kambi hasa kwa kuegemea kwenye
maeneo kama nguvu ya fedha katika kufadhili harakati za siasa, kukomaa
kwa demokrasia, umakini na uwezo wa viongozi wake na kubwa zaidi, wingi
au uhakika wa wanachama katika maeneo mbalimbali.
Nguvu ya fedha
Kigezo cha nguvu ya fedha ni muhimu kwani ndilo eneo linalochangia ushindi kwa kiwango kikubwa katika siasa za ushindani.
Fedha ndiyo inayowezesha viongozi kutembelea maeneo mbalimbali nchini kujinadi na kutafuta uungwaji mkono.
Kwa Tanzania, vyama vyote vinavyoshiriki katika
uchaguzi vinakidhi kigezo hiki, japo kwa uwezo tofauti. Kwa mfano,
vyote vinapata ruzuku kutoka serikalini.
Hata hivyo, CCM ndiyo inayoongoza kwa kupewa kiasi
kikubwa cha fedha kama ruzuku. Wakati CCM ikipata ruzuku ya takriban
Sh800 milioni kwa mwezi, Chadema inapata Sh203.6 milioni huku CUF
ikipata Sh117.4 milioni na NCCR-Mageuzi Sh10 milioni.
Ukiachilia mbali kiasi kikubwa cha fedha za ruzuku
inachopata CCM, bado chama hicho kina sifa ya nyongeza kulinganisha na
upinzani, kwani ndicho chama chenye vitegauchumi vingi na wafadhili
wengi wakiwamo wafanyabiashara wakubwa nchini.
Mtandao wa wanachama
CCM pia inao mtaji wa wanachama nchi nzima kutokana na mtandao wake kilioujenga tangu wakati wa mfumo wa chama kimoja.
Ni CCM iliyoanzisha mfumo wa uongozi katika ngazi ya shina
(mabalozi wa nyumba kumi), mtindo unaokiwekea mazingira mazuri ya
kujikusanyia wanachama wa uhakika katika maeneo mengi ya nchi, hususan
vijijini ambako upinzani umeshindwa kupenya kwa kiasi kikubwa.
Mfumo huu wa uongozi wa mashina umeigwa na
Chadema. Hata hivyo, mafanikio yake hayalingani na ya chama hicho
kikongwe kilichojikita mizizi kwa muda mrefu.
Demokrasia ndani ya vyama
Licha ya kuwapo kelele za matumizi makubwa ya
fedha na vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi, mfumo wa uongozi wa
chama hicho tawala unaonekana kuwa wa kidemokrasia kulinganisha na ule
wa vyama vya upinzani.
Ni CCM ndiyo inayoonekana viongozi wake wakiachiana madaraka kwa njia ya kidemokrasia kila baada ya miaka fulani.
Wakati CCM ikiweka bayana katika Katiba yake
vipindi viwili vya uongozi, kwa vyama vya upinzani hakuonekani kuwapo
kwa demokrasia hiyo, baadhi yao tangu vianzishwe viongozi wa kitaifa ni
walewale. Vyama vyote vinavyounda Ukawa havina ukomo wa madaraka na
viongozi wake wote wa taifa, wamedumu katika kwenye uongozi kwa zaidi ya
vipindi viwili vya miaka mitano.
Wasemavyo wachambuzi
Mhadhiri mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Profesa Kitila Mkumbo anasema pamoja na ukweli kuwa CCM inaweza
kuvizidi vyama vya upinzani katika kila eneo, bado upinzani una nafasi
kubwa ya kufanya vizuri na hata kushinda katika uchaguzi ujao.
Anasema kwa hali ilivyo sasa, wananchi wengi
wamechoshwa na matukio mengi yasiyofaa yanayofanywa na viongozi wa
Serikali iliyopo madarakani na wanachotaka ni mabadiliko.
Anasema licha ya kuwapo kwa matatizo katika mifumo
ya uongozi ndani ya upinzani, ikiwamo kuminywa kwa demokrasia,
wananchi wengi wanataka mabadiliko na wapo tayari kuing’oa CCM.
Kuhusu kigezo cha fedha na mtandao wa uongozi,
anasema mambo hayo hayawezi kuwa kigezo cha ushindi kwa CCM, kwa sababu
kwa hali ilivyo sasa vyama vya upinzani navyo vina fedha nyingi na
vinaweza kuzitumia kuwafikia wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi.
“Kwa mfano, Chadema wana pesa nyingi zinazowawezesha kuzunguka mikoani kujijenga na kujiimarisha,” anasema.
Mchambuzi wa masuala ya siasa na utawala bora nchini, Buberwa
Kaiza anasema ni vigumu kutabiri chama kipi kitashinda uchaguzi katika
kipindi hiki, kwa kuwa ushindi wa chama utategemea na mgombea
atakayesimamishwa.
Anasema ni kweli, CCM inaonekana kujijenga tangu chini, lakini kilikuwakimejengwa na vyama vya ushirika ambavyo sasa vimekufa.
Anasema vyama vya upinzani kupitia Ukawa,
vinaonekana kuungwa mkono zaidi na watu wa mijini na wasomi kwa kiasi
fulani. Anasema kwa sasa ni vigumu kutabiri ushindi wa Ukawa kwa kuwa
umoja huo haujaweka bayana jina la mgombea wake.
‘’CCM wameshuka kiasi fulani na upinzani umepanda
kwa kiasi fulani, tukifikia wakati vyama vikaweka wagombea wake
hadharani, labda ndipo watu watakuwa na uamuzi,’’ anasema.
Kuhusu suala la nguvu ya fedha, Kaiza anasema
ingawa CCM inaonekana kuwa na fedha nyingi, ukweli ni kuwa ndani ya
vyama watu ndiyo wenye fedha na siyo za vyama.
“Siamini kuwa CCM wana fedha watakazozitumia
wakati wa uchaguzi na siamini kuwa wapinzani nao hawana fedha kabisa.
Ninachojua ni kuwa hawa wenye fedha watazipeleka pale wanapoona kuna
ushindi,’’ anaeleza.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard
Mbunda anakubaliana na vigezo vinavyokipa chama tawala nafasi ya kufanya
vizuri, lakini anasema endapo Ukawa itasimamia mpango wake wa kuungana
na kuwa kitu kimoja katika uchaguzi mkuu ujao, umoja huo unaweza kufanya
maajabu.
“Naamini wapinzani wanaweza kuleta upinzani wa
maana na juhudi zao zinaweza zikawa kigezo kikubwa cha kuufanya upinzani
ushinde,” anasema.
No comments:
Post a Comment