Dar es Salaam. Licha ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda) kukusanya cha Sh1.78 bilioni kwa mwezi, wafanyakazi wake wamelalamikia uongozi wa shirika hilo kushindwa kuwalipa mishahara kwa kipindi cha miezi minne.
Sambamba na madai hayo, pia Uda wanadaiwa kutowapa wafanyakazi hao ufafanuzi wa ukokotozi wa makato ya kodi na mifuko ya hifadhi ya jamii.
Hata hivyo, Msemaji wa shirika hilo, George Maziku alisema wafanyakazi hao hukatwa kiasi cha Sh130,000 kama kodi sambamba na NSSF, hivyo wanapaswa kuuliza uongozi na siyo kwenda kulalamika pembeni.
Wakati msemaji huyo akisema hivyo, jana wafanyakazi hao walidai kuwa hawajalipwa mishahara yao ya Januari na Februari licha ya kufanya kazi kwa saa 20 kwa siku.
“Tunalipwa Sh400,000 kwa mwezi kama mashahara, lakini tunakatwa zaidi ya Sh130,000 ambayo tunaambiwa kwamba ni malipo ya kodi ya Serikali, lakini haionekani kwenye hati ya malipo ya mshahara,” alisema mmoja wa wafanyakazi hao ambaye hata hivyo hakuwa tayari kutaja jina lake.
Mfanyakazi mwingine alilalamikia mishahara midogo na kusema kuwa wapo wafanyakazi wanaolipwa kuanzia Sh16 milioni kwa mwezi.
Jumla ya kiasi kinachokusanywa ni karibu Sh1.78 bilioni.
“Kila tukimweleza mkuu wetu anatuambia hakuna wa kumtisha, watoto hawajaenda shule tangu Januari tunadaiwa ada, nyumba tunazoishi wengine wamefukuzwa familia,” alisema mmoja wa madereva wa Uda.
Akijibu tuhuma hizo msemaji huyo alisema, “Mishahara wanayodai ni wa mwezi Februari pekee,” na alipoulizwa kwa nini wafanyakazi hawapewi karatasi za malipo zenye ukokotoaji na malalamiko ya kutowasilisha fedha zao NSSF alisema: “Hilo ni suala la wao kuzungumza na uongozi na si kwenye vyombo vya habari .” Kuhusu muda wa kufanya kazi, Maziku alisema wafanyakazi hao hawajapangiwa saa za kufanya kazi, bali kiasi cha fedha za kuwasilisha Uda kwa siku.
Msemaji huyo alisema, aliwataka wafanyakazi hao kukutana na kujadiliana na uongozi wa shirika badala ya kukimbilia katika vyombo vya habari kwa ajili ya kupata suluhisho.
No comments:
Post a Comment