Yanga yatuliza kichwa mbele ya Mgambo - LEKULE

Breaking

21 Mar 2015

Yanga yatuliza kichwa mbele ya Mgambo



Dar es Salaam.
Yanga inaikabili Mgambo Shooting leo kwenye Uwanja wa Mkwakani Tanga, huku ikihitaji ushindi ili izidi kuikimbia Azam FC inayofukuzana nayo kileleni.

Yanga inaongoza ligi kwa kuwa na pointi 34, wakati Azam ni ya pili ikiwa na pointi 33 na inacheza kesho kweye Uwanja huohuo dhidi ya Coastal Union.

Timu hizo zinafukuzana kwa kasi kwani kila moja inautaka ubingwa msimu huu, Azam ikitaka kutetea ubingwa wake iliyoupata msimu uliopita, wakati Yanga wakitaka kurejesha ubingwa waliopokonywa na Azam FC.

Yanga inaikabili Mgambo ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 2- 1 ilioupata dhidi ya Kagera Sugar wiki iliyopita, lakini haitakuwa kazi rahisi kuwakabili maafande hao kwani mara kwa mara wamekuwa wakipata wakati mgumu kushinda kwenye uwanja huo.

Ushindi walioupata Yanga dhidi ya Coastal Union mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani unaweza ukawapa kiburi na kuona kuwa wanaweza hata kushinda leo dhidi ya Mgambo kwani tayari wameshaondoa ‘gundu’.

Ugumu wa mchezo huo unakuja kutokana na Mgambo kuifunga Simba mabao 2-0 mwishoni mwa wiki iliyopita, hivyo wataingia uwanjani wakiwa na morali na wakijiamini, pia watajiamini zaidi kwani msimu uliopita maafande hao waliibuka wababe wa Yanga kwenye uwanja huohuo kwa kuwabamiza mabao 2-1.

Yanga itakuwa na ahueni baada ya wachezaji wake sita iliowakosa katika mchezo uliopita kutokana na kuwa na kadi wote kurejea kikosini leo.

Kelvin Yondani, Said Juma, Danny Mrwanda wote walikuwa na kadi tatu za njano, wakati Haruna Niyonzima alikabiliwa na adhabu ya kadi nyekundu, lakini wote leo watarejea kuongeza nguvu katika mchezo wa leo.

Kocha wa Yanga, Hans Pluijm alikiri mchezo wa leo kuwa mgumu lakini anawaamini wachezaji wake watamfanyia kazi nzuri itakayowapa ushindi.

“Nina kikosi kizuri chenye wachezaji bora, wiki iliyopita tuliwakosa wachezaji wengi kutokana na sababu mbalimbali, lakini tukashinda dhidi ya Kagera kwa sababu waliobaki walifanya kazi yao vizuri, hivyo naaamini hata kesho ( leo) tutashinda.

“Kikubwa ni wachezaji kuwa na nidhamu ya mchezo, ili tuweze kushinda, najua kutakuwa na changamoto ya uwanja kwani hauko katika hali nzuri, lakini tutapambana kuhakikisha tunaondoka na pointi zote tatu,” alisema Pluijm.

Kocha huyo Mholanzi ataendelea kumkosa winga Mbrazili, Andrey Coutinho anayesumbuliwa na maumivu wa goti, lakini nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ aliyekuwa na mshono juu ya jicho yuko fiti kuwavaa Mgambo leo.

Kocha wa Mgambo, Bakari Shime alisema wapinzani wao wanatakiwa kujipanga na kuwa tayari kupokea kipigo kama walichopata watani zao wa jadi, Simba.

“Sisi tumejiandaa na hatuna wasiwasi na mechi hiyo, tunawaheshimu Yanga ni timu kubwa lakini tutahakikisha tunawafunga kama tulivyowafunga Simba,” alisema Shime.

Mgambo imekuwa na matokeo mazuri nyumbani dhidi ya Simba na Yanga, kwani walikuwa wababe katika michezo yote ya msimu uliopita kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani.

No comments: