Lema: Kinana amepigwa changa la macho Arusha - LEKULE

Breaking

23 Mar 2015

Lema: Kinana amepigwa changa la macho Arusha

Kama mimi ni mwizi na tapeli, hivi hata usalama wanashindwa kuwaeleza ukweli washughulike na mimi? Ndiyo maana watu tuliowafukuza Chadema wamewapokea eti wamehama chama. Wameingizwa mjini hao,” Lema



Arusha. 
Siku moja baada ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kuwapokea viongozi wawili akisema wanatoka Chadema na kumtuhumu Mbunge wa Arusha, Godbless Lema kuwa anatumia madaraka yake kujinufaisha na mali za umma, mbunge huyo amejibu akisema: “Kinana amepigwa changa la macho.”

Akiwa Arusha mwishoni mwa wiki Kinana aliwapokea waliokuwa wenyeviti wa Chadema katika Wilaya ya Monduli, Amani Silanga na wa Ngorongoro, Revocatus Palapala lakini jana Lema alisema viongozi hao walikwishatimuliwa Chadema tangu mwaka 2013.

Kinana alisema migogoro ya CCM ndiyo iliyokinufaisha Chadema na Lema akaingia madarakani, lakini akawataka wananchi kujutia uamuzi huo na kutorudia kumchagua mbunge huyo.

“Mbunge wenu ameshindwa kutekeleza kile mlichomtuma bungeni badala yake anatumia madaraka yake kujimilikisha mali za umma na kutukana hovyo,” alisema na kuongeza:

“Mfano ni lile shamba alilopewa na Mayala ambalo ameliuza, trekta na vifaa vingine vyote ameviuza lakini migogoro ya ardhi na maji ameshindwa kuitatua.”

Majibu ya Lema

Akijibu tuhuma hizo, Lema alisema Kinana amepigwa ‘changa la macho’ na amefanyiwa maigizo kama ya futuhi na watu wa usalama wameshindwa kumwambia ukweli.

Alisema mambo yote aliyoambiwa ni uongo mtupu ambao yeye hawezi kusumbuka nao.

“Kama mimi ni mwizi na tapeli, hivi hata usalama wanashindwa kuwaeleza ukweli washughulike na mimi? Ndiyo maana watu tuliowafukuza Chadema wamewapokea eti wamehama chama. Wameingizwa mjini hao,” alisema.

Alisema: “Silanga na Palapala walifukuzwa tangu Novemba 30, 2013 baada ya kubainika kuwa kwenye mtandao wa Zitto na wote walitimkia ACT kama walivyofanya kina Mwigamba (Samson) na Kitila Mkumbo,” alisema Lema akitoa nakala ya taarifa kwa vyombo vya habari.

Alisema baadaye Silanga na Palapala walijiunga CCM na Palapala aligombea na kushinda uenyekiti wa Kijiji cha Wasso wilayani Ngorongoro kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa Desemba 14, mwaka jana.

“Ni maajabu ya mwaka mwenyekiti wa kijiji kupitia CCM tangu Desemba 14, mwaja jana, apokewe na Kinana akitangazwa kukihama Chadema?” alisema Lema.

Mbunge huyo alisema taarifa kwa vyombo vya habari ya Novemba 30, mwaka juzi, iliyosainiwa aliyekuwa Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa na habari iliyoandikwa kwenye gazeti la Daily News la Desemba 2, 2013, vyote vinaelezea kufukuzwa kwa Silanga.

Staili ya Kinana

Staili ya kukemea ufisadi katika vyama vya siasa ikiwamo CCM juzi ilimbeba Kinana na kujikuta akishangiliwa wakati wote jijini Arusha, mahali ambako kulikuwa na hofu ya kukosa watu wa kutosha.

Kinana aliingia jijini Arusha mwishoni mwa wiki na alitumia siku nzima ya Ijumaa akizunguka katika maeneo mbalimbali akitembea kwa miguu na kuzungumza na wananchi.

Katika maeneo aliyokuwa akipita, Kinana alihubiri habari za kupambana na mafisadi, jambo lililomfanya akubalike na watu wengi kumsikiliza kwa kuwa walionekana kuguswa zaidi na hotuba hizo.

Juzi, wananchi walijitokeza kwa wingi katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid kumsikiliza na muda wote aliohutubia umati wa watu.

Kwenye mkutano huo, Kinana alianza kwa staili ya kukemea mafisadi akisema wako kila chama na kuwataka Watanzania kuungana pamoja na kuwafichua kwa nguvu zote bila ya kujali itikadi.

Katibu huyo alieleza kuwa ndani ya CCM kuna baadhi ya watu ambao ni mafisadi na chama hakiwezi kuwavumilia kwa kuwa kazi yake ni kusimamia misingi bora iliyoachwa na waasisi wake.

“Lakini hata Chadema na vyama vingine wako mafisadi tena wengi, ndiyo... fisadi ni fisadi haijalishi anatoka chama gani lakini akiwa fisadi hajifichi. Watu wa aina hiyo hawafai kuwa viongozi, hawafai kwa kupewa nafasi yoyote maana hao wanapenda kula na wakipewa nchi wanaweza kuleta ubaguzi mkubwa katika masuala ya kimaendeleo.”

Kinana alisema mpango wa kuwalea wezi na wala rushwa umefika mwisho na hauwezi kuvumilika tena ndani ya CCM na akaomba vyama vingine navyo vianze kupambana na mambo ya aina hiyo.

Alisema katika maeneo yote viongozi wa juu ndiyo walafi na wapenda rushwa wakitumia nafasi zao kuliko wale wa ngazi ya chini ambao wengi wanakuwa na hofu.

Matunda ya ziara

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alizungumzia mafanikio ya ziara hiyo iliyotokana na maagizo ya Mkutano Mkuu wa CCM ulioagiza watendaji wa chama kutembelea wanachama wao kuwa imeongeza uwajibikaji na kwamba wanaosema ziara hizo hazifai ni wale wenye malengo yao tofauti na chama.


No comments: