Kumekucha urais 2015 - LEKULE

Breaking

23 Mar 2015

Kumekucha urais 2015

Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa akiwasalimia wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali vya mjini Dodoma na waendesha bodaboda walioandamana kwenda nyumbani kwake mjini humo jana kwa ajili ya kumshawishi achukue fomu ya kuwania Urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Picha na Anthony Siame


Arusha/Dodoma/Mbeya.
Kadri uchaguzi mkuu unavyokaribia ndivyo makundi mbalimbali ya jamii yanavyoibuka kwa staili tofauti za kuwashawishi  baadhi ya makada ili watangaze nia ya kuwania urais ndani ya CCM.

Makundi hayo yalianza kwa kumshawishi Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa na sasa yameibuka mengine katika mikoa ya Mbeya na Arusha yakiwashawishi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.

Hata hivyo makundi hayo yameelezwa na mmoja wa watu waliotangaza kuwania nafasi hiyo kuwa ni mbinu ya kimaigizo ya baadhi ya wagombea kujitangaza kwa kuyaandaa na kuyalipa posho.

Wanafunzi watinga kwa Lowassa

Siku moja baada ya kuwapokea masheikh 50 kutoka Bagamoyo, jana mbunge huyo alipokea makundi ya wanafunzi wa vyuo vikuu, madereva wa pikipiki (bodaboda) na wamachinga wa Dodoma wakimtaka achukue fomu kuwania nafasi hiyo.

Tayari mbunge hiyo alishampokea Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Dk Rapahel Chegeni na baadaye kundi marafiki wa Lowassa kutoka mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha.

Wanafunzi hao ambao waliongozana na baadhi ya wahadhiri walitoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), St John, Mipango na Chuo cha Biashara (CBE), Tawi la Dodoma.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti nyumbani kwake mjini hapa jana, wanafunzi hao walimtaka Lowassa kuchukua fomu ya kuwania urais wakati utakapofika.

“Sisi hatutafuni maneno, ni watu wawazi na tuna tamaa kwa mtu ambaye tuna matumaini naye na mtu ambaye tuna matumaini naye ni wewe Lowassa,” alisema Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Wazazi la CCM Kusini Unguja, Haji Amiri na kuongeza:

“Watanzania wana matumaini na wewe.  Sasa yeyote anayetaka kuyafunika matumaini yale ni sawa na kukiuka matumaini yetu.”

Kiongozi wa madereva Bodaboda, Bakari Ndalama alisema yeye na wenzake walifika kumuomba kugombea nafasi hiyo kwa sababu akichukua, hali ya ajira itakuwa nzuri.

“Wewe umekuwa ukilisemea jambo hili mara kwa mara. Ukipata urais ajira zitakuwa nzuri kwa vijana,” alisema Ndalama.

Rais wa Serikali ya Wanafunzi UDOM, Fredrick Lutenalo alisema wanamuunga mkono Lowassa na wamejipanga kumsaidia hadi dakika za mwisho... “Wakati ukifika wa kuchukua fomu, uchukue kwa ujasiri bila kuogopa na tutakusindikiza.”

Hali ilivyokuwa

Makundi yalifika nyumbani kwa Lowassa kwa maandamano huku yakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali na kuimba nyimbo za kuhamasishana.

Baadhi ya mabango yalikuwa yameandikwa “4U Movement Friends of Lowassa”; “walitunyima elimu ukatupatia shule za kata na Chuo Kikuu cha Dodoma.”

“CCM tupatie Lowassa nafasi ya urais mwaka 2015.

kutokana na hali hiyo, baadhi ya majirani walitoka nje ya nyumba zao ili kutazama kinachoendelea wakati kundi hilo lililokuwa na watu zaidi ya 300 lilipoingia ndani ya nyumba hiyo.

Kutokana na wingi wa watu na udogo wa eneo, iliwalazimu waandamanaji hao kubanana ili waweze kusikilizana, wakati walipopewa nafasi ya kuzungumza.

Kauli ya Lowassa

Akizungumza na makundi hayo, Lowassa alisema Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu utakuwa mgumu, hivyo kuwataka wanaomshawishi kuwania urais, kuwashawishi pia watu kujiandikisha kwa wingi katika daftari la wapiga kura.

“Uchaguzi huu utakuwa mgumu sana na utakuwa na mambo mengi sana, lakini uchaguzi ni mahesabu,” alisema.

Bila kufafanua, Lowassa ambaye juzi alipotembelewa na masheikh 50 kutoka Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani alieleza kushawishika kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi huo, alisema hadi kufikia juzi, watu zaidi 800 walifika kumshawishi kuwania nafasi hiyo.

Profesa Mwandosya

Mbali na Lowassa, shirikisho la wanachama wa CCM katika vyuo vikuu viliyopo jijini Mbeya limetangaza kumshawishi Waziri Profesa Mwandosya naye atangaze nia ya kuwania urais muda utakapofika.

Viongozi wa shirikisho hilo wakiongozwa na katibu wake, Oscar Mwaihabi walisema wameamua kujitosa kumshawishi Profesa Mwandosya kwa imani kwamba anao uwezo mkubwa na pia hana tuhuma zinazoweza kukiathiri chama wakati wa kampeni.

Akisoma tamko lao jana kwenye Ukumbi wa Benjamin Mkapa huku akiwa na vijana waliojitambulisha kuwa wanatoka vyuo vya Tumaini, Teofilo Kisanji (Teku), Mzumbe, Saut na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia (Must), Mwaihabi alisema:

“Profesa Mwandosya ni msomi mwenye upeo wa kuongoza Taifa vizuri katika masuala ya siasa, uchumi na kijamii pia hana tuhuma ambazo zitasababisha CCM itumie muda mrefu kumsafisha wakati wa kampeni.”

Katika taarifa yao, wana vyuo hao walitumia kauli iliyowahi kutolewa na Dk Chegeni wakati akimshawishi Lowassa, kuwa wametangaza hayo katika kutekeleza kauli ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete ambaye alisema wapo viongozi wazuri ambao wanatakiwa kushawishiwa.

“Profesa Mwandosya unafaa kabisa kuwa rais, tofauti na wengine wanaotajwa kwa sababu ni mchapakazi, mwadilifu na huna kashfa mbaya katika jamii, hivyo tunaomba ujiandae kuchukua fomu muda ukifika,” alisema.

Awali, Katibu Mwenezi wa shirikisho hilo, Julius Mambo aliwataka wana vyuo kushikamana kumshauri Profesa Mwandosya kuchukua fomu.

Majibu ya Mwandosya

Alipoulizwa kwa simu jana, Profesa Mwandosya ambaye hakuwapo katika mkutano huo alisema: “Siwezi kuzungumza mengi kwa sasa, ninawashukuru kwa dhati hao wanafunzi, wakati utakapofika nitazingatia ushauri wao.

Profesa Muhongo

Juzi, umoja wa wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro nao umeibuka na kutangaza kumuunga mkono na kumshawishi aliyekuwa waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuchukua fomu.

Siku moja baada ya wanafunzi kutangaza hatua hiyo, Profesa Muhongo aliyejizulu uwaziri kwa kushindwa kushughulikia vyema kashfa ya Tegeta Escrow, alijibu akisema amesikia na tayari amefikia uamuzi atakaoutangaza kipenga kikipulizwa.

kupitia kwa mwenyekiti wao, Charles Ngereza wanafunzi hao waliwaambia waandishi wa habari jijini Arusha kuwa watazunguka kwenye vyuo na taasisi zote za elimu ya juu nchini kuwashawishi wenzao kuungana nao.

“Sababu kuu ya kumuunga mkono ni rekodi ya utendaji wake. Kwa kipindi kifupi alichoongoza Wizara ya Nishati na Madini amefanya mapinduzi makubwa yaliyowashinda watangulizi wake ikiwamo kushusha bei ya kuunganisha umeme kufikia kati ya Sh27,000 hadi 177,000 vijijini,” alisema Ngereza.

Alisema kasi ya utekelezaji wa mradi wa umeme vijijini, licha ya kuwapatia wananchi huduma ya nishati, pia imechangamsha uchumi vijijini kwa kuongeza shughuli za uzalishaji zinazotegemea nishati ya umeme.

Akizungumza mbele ya wawakilishi kutoka vyuo vikuu vya Tumaini Makumira, Semmco, Jomo Kenyatta, Mount Meru na Uhasibu Arusha (IAA), mwenyekiti huyo alitaja sifa nyingine ya Profesa Muhongo kuwa ni jasiri wa kusema na kutenda akitolea mfano alipozuia udalali katika sekta ya gesi na mafuta.

Wanafunzi waliohudhuria mkutano huo na vyuo vyao kwenye mabano ni Rahma Sengela (Jomo Kenyatta), Daudi Shayo (IAA), Sarah Aminarabi (Arusha), Nelson Machumu (Semmco) na Hobeshi Juvenary kutoka Makumira.

Kuhusu Profesa Muhongo kujiuzulu kwa kashfa ya Escrow, Ngereza alisema hatua hiyo ilitokana na uwajibikaji wa kubeba dhamana jambo lilipoharibika katika eneo analoongoza.

Alisema hiyo ni moja ya sifa za uongozi na kumtaja Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi aliyejiuzulu uwaziri wakati wa uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere na baadaye kuukwaa urais.



Msimamo wa Profesa Muhongo

Akizungumza kwa simu kuhusu kauli ya wanafunzi hao, Profesa Muhongo alithibitisha kuombwa na makundi kadhaa ya kijamii wakiwamo wazee wa mikoa ya Kanda ya Ziwa na tayari ametafakari na kufikia uamuzi ambao alisema atautangaza mara baada ya chama chake, CCM, kupuliza kipenga cha uchaguzi.

“Nimeshafanya uamuzi kuhusu suala ya urais katika uchaguzi ujao. Ninachosubiri ni chama kutangaza ratiba ya uchaguzi ili niutangazie umma uamuzi wangu,” alisema Profesa Muhongo.

Kuhusu kuunda timu au mtandao wa kampeni, Profesa Muhongo alisema: “Sina timu wala mtandao binafsi. Timu yangu na mtandao wangu ni Taifa la Tanzania na nachukua fursa hii kuwaomba Watanzania kukataa kugawanywa na makundi kwenye masuala yenye masilahi kwa Taifa kama kumchagua rais wa nchi.”

January Makamba akerwa

Kutokana na makundi hayo kujitokeza kila kukicha kuwashawishi wanaowania urais, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba ameyakosoa akisema nafasi ya urais ni ya hadhi na heshima kubwa, inapoombwa haipaswi kufanyiwa michezo ya kuigiza.

“Huu utaratibu wa kuratibu watu, kuwasafirisha, kuwapa posho na ubwabwa waje kukuomba kugombea ni michezo ya kuigiza ambayo ni aibu kubwa,” alisema.

Alisema kila mgombea ana uwezo wa kutengeneza watu wa kumuomba kugombea lakini wengine hawafanyi hivyo kwa sababu wanaheshimu nafasi wanayoiomba na wanaamini kwamba haipaswi kutafutwa kwa ulaghai na maigizo.

“Ni aibu sana kutumia shida na njaa za watu kisiasa. Ni aibu sana kukusanya vijana na wazee wa watu na kuwapangia viti na mahema na kuwapa pesa na kuwapiga picha. Ukiona mtu anatafuta nafasi ya uongozi kwa ujanja na ulaghai, ujue atatawala kwa ujanja na ulaghai,” alisema Makamba bila kutaja jina la mgombea yeyote.

Mbunge huyo wa Bumbuli ambaye tayari ametangaza nia yake ya kuwania urais, alisema mgombea anayehaha na kutumia fedha nyingi kuonyesha anakubalika hajiamini.

“Kama unakubalika huwezi kuratibu makundi na kuyalipa na kuwapiga picha na kuita waandishi wa habari waje kushuhudia, hizo ni mbinu za mfa maji,” alisema na kuongeza:

“Naamini chama changu hakitatishwa na nguvu za maigizo. Tunataka uongozi safi unaomuogopa Mungu. Tunataka uongozi wenye uadilifu na fikra mpya za kuisogeza mbele Tanzania. Tunataka viongozi watakaomaliza shida za Watanzania, siyo wanaozitumia shida hizo kisiasa.”

Januari alikwenda mbali akitoa mfano wa baba yake, Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, akisema: “Hata Mzee Makamba, pamoja na umri wake wa miaka 75, leo akiwa na pesa za kumwaga anaweza kutengeneza makundi yakamuombe kugombea urais.

“Ifike mahali katika nchi yetu tuache hii michezo. Tukiendelea na mambo haya, tunatengeneza Taifa linaloendeshwa kwa propaganda tu. Watu wanaotaka kuomba nafasi ya urais wanapaswa kuwa na ujasiri na wanapaswa kujiamini na kusema wanataka nafasi hiyo na wana fikra gani mpya bila kutumia pesa kuonyesha kwamba wanagombea kwa sababu wanahitajika na watu. Uongozi thabiti na shupavu hautokani na michezo ya kuigiza.”

No comments: