WATU wa El Merreikh mjini Khartoum,
Sudan wamewaambia Azam FC, hata
waende kulalamika wapi, Shirikisho la Soka
Afrika haliwezi kuwasikiliza kwa kuwa kuna
mtu anaitwa Magdi Shams El Din (pichani
juu).
Azam FC jana imeaga mashindano ya Ligi
ya Mabingwa Afrika, baada ya kufungwa
mabao 3-0 na El Merreikh ya Sudan katika
mchezo wa marudiano wa Raundi ya Awali
uliofanyika Uwanja wa Marreikh mjini
Khartoum.
Marefa wa mchezo huo kutoka Zambia
Wellington Kaoma aliyesaidiwa na Romeo
Kasengele na Amos Nanga walionekana
wazi kuiuma Azam FC katika mchezo huo.
Pamoja na kupewa penalti ambayo ilipigwa
na Augustine Okran na kuokolewa na kipa
Aishi Manula, Merreikh ilimaliza dakika 45
za kwanza inaongoza kwa bao 1-0
lililofungwa ba Bakr dakika ya 16.
Kipindi cha pili marefa wa Zambia
waliongeza mbeleko kwa Merreikh na
ikafanikiwa kupata mabao mawili zaidi
yaliyofungwa na Ahmed Abdallah dakika ya
85 na Alan Wanga dakika ya 90.
Azam FC inatolewa kwa jumla ya mabao
3-2 baada ya awali kushinda 2-0 katika
mchezo wa kwanza nyumbani, Uwanja wa
Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Kwa kujua mbinu walizopanga na marefa
hao, Merreikh walizuia mchezo huo
usionyeshwe na Televisheni yoyote.
Na baada ya mchezo huo, Azam FC
walianza jitihada za kuwasilisha malalamiko
yao kwa Kamisaa, Ahmed Mohamed
Magahed Osman wa Misri lakini
hawakusikilizwa.
Kamisaa huyo alikuwa akiongea kwa
kicheko na furaha na viongozi wa Merreikh
na watu wa timu hiyo ya Sudan
wakawaambia kwa Kiingereza viongozi wa
Azam FC; “Mtakwenda popote
hamtafanikiwa, kuna Magdi Shams El Din,”.
Magdi Shams El Din ni Msudan, ambaye ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Marefa ya
Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ambayo
inahusika kupanga marefa kwenye
mashindano.
Hakuna refa ambaye anaweza kupuuza
agizo la Magdi Shams El Din kwa sababu
anajua ataishia kuchezesha Ligi za nchini
mwao na kwa sababu hiyo kuna uwezekano
marefa wa Zambia waliweka pembeni sheria
17 za soka katika mchezo wa jana ili
‘kumfurahisha’ bosi wao, Magdi Shams El
Din.
Lakini pamoja na ‘mikwara’ hiyo, Mtendaji
Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba mwenye
uzoefu wa kuanzia kufanya kazi Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF) amesema
wanapelekea kesi na ushahidi wote CAF juu
ya udhalimu waliofanyiwa na Merreikh na
marefa wa Zambia.
Kwa ujumla, matendo yote waliyofanyiwa
Azam FC nchini Sudan toka siku ya kwanza
walipowasili nchini humo hayakuwa ya
kisoka na yamefananishwa na matendo ya
kigaidi ndani ya mchezo wa soka.
Ikumbukwe pia siku walipofika walipokewa
na longolongo nyingi uwanja wa ndege na
walisumbuliwa sana ikiwa ni pamoja na
kucheleweshewa visa zao, lakini pia hata
gari walilopokelewa lilikuwa ni bovu sana
kama vilie la kubebea mkaa.
No comments:
Post a Comment