HOMA YA MECHI YA WATANI,SIMBA YAWEKA KAMBI ZANZIBAR - LEKULE

Breaking

2 Mar 2015

HOMA YA MECHI YA WATANI,SIMBA YAWEKA KAMBI ZANZIBAR



Zikiwa zimebaki siku saba katika ya mechi ya watani wa jadi nchini, Simba SC na Yanga SC, Wekundu wa Msimbazi wamekimbilia Zanzibar kusaka mbinu za kuiua Yanga SC.
Simba SC na Yanga SC zitakutana Uwanja wa Taifa jijini hapa Jumapili kwa ajili ya mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Taarifa ambazo mtandao huu umezipata kutoka ndani ya uongozi wa Simba SC jijini hapa muda mfupi uliopita, zimeeleza kuwa kikosi cha Mserbia Goran Kopunovic kimepanda boti jioni ya leo kwenda Zanzibar kuwanolea makali Yanga SC.
Simba SC ambayo jana ilishinda 5-0 dhidi ya Tanzania Prisons FC Uwanja wa Taifa, kikiwa ni kipigo kikubwa zaidi msimu huu, inakamata nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 23, moja nyuma ya Kagera Sugar FC katika nafasi ya tatu, nne nyuma ya Azam FC katika nafasi ya pili na nane nyuma ya Yanga SC wanaoongoza msimamo.
Simba SC imekuwa na utaratibu wa kuweka kambi Zanziba na maeneo mengine nje ya Dar es Salaam inapokaribia kucheza dhidi ya Yanga SC.
Yanga SC nao wamekuwa na uataribu huo wa kuweka kambi nje ya Dar es Salaam wakijificha mara nyingi katika maeneo ya Bagamoyo, Pwani na kisiwani Pemba kabla ya kumvaa mnyama.

No comments: