Hatua kali kwa wanaharakati waliokamatwa DRC - LEKULE

Breaking

16 Mar 2015

Hatua kali kwa wanaharakati waliokamatwa DRC

Waandishi wa habari wa kigeni, wanadiplomasia, wanaharakati na wasanii mbalimbali wametiwa mbaroni na polisi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wakiwemo waandishi wa habari wa BBC.
Wanaharakati hao, ambao ni vijana kutoka nchini Burkina Faso, Senegal na Congo, walikuwa na mkutano na waandishi wa habari kuhusu jukwaa jipya la kijamii.
Mwandishi wa BBC Maud Jullien ametutumia taarifa inayosomwa na Ben Mwang'onda.
Msemaji wa serikali na ambaye pia ni Waziri wa Habari Lambert Mende amesema wanaharataki ambao wanaozuiliwa waliletwa ndani ya nchi ili kuongoza maasi dhidi ya serikali.
Wanaharakati hao ni raia watatu kutoka Senegal , mmoja wa Bukina Faso na wengine 14 raia wa Congo.
Walifumaniwa na jeshi la polisi na kukamatwa wakati wakiwa kwenye mkutano na waandishi wa habari.
Duru kutoka kwa serikali ya Congo zimeambia BBC kwamba watamrejesha nyumbani afisa mmoja wa ubalozi wa Marekani aliyeshiriki mkutano wa Jumapili.
Ubalozi wa Marekani mjini Kinshasa umekiri kufadhili mkutano huo ambao uliwaleta pamoja vijana wanaharakati ili kubadilishana mawazo.

Hata hivyo ubalozi huo haujadthibitisha ikiwa afisa wake Sturr atarejeshwa nyumbani.
BukinaFaso na Senegal zimeshuhudia maandamano ya raia kuwapinga viongozi wanaongangania madaraka kinyume cha katiba za nchi hizo.
Rais wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila anatarajiwa kukamilisha muhula wake mwaka 2016.
Mapema mwaka huu zaidi ya watu 40 waliuawa kwenye maandamano ya raia kupinga mswada ambao ungewezesha Rais Kabila kuongeza muhula wake.

No comments: