Urais 2015: Wana CCM Waanza Kushikana Uchawi.....Wadai kuwa Jukumu la Kupata Mgombea wa Chama Siyo la kifamilia bali ni la Wanachama Wote - LEKULE

Breaking

23 Feb 2015

Urais 2015: Wana CCM Waanza Kushikana Uchawi.....Wadai kuwa Jukumu la Kupata Mgombea wa Chama Siyo la kifamilia bali ni la Wanachama Wote


Wakati  CCM kikijiandaa kuanza mchakato wa kupitisha jina la mgombea wake wa nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu, imeelezwa kwamba hali si shwari ndani ya chama hicho kutokana na kile kinachodaiwa, mkakati wa baadhi ya viongozi kubeba na kukumbatia watu wao kwa lengo la kulinda masilahi binafsi.
 
Chanzo chetu cha kuaminika kutoka ndani ya CCM kimeeleza kuwa joto kubwa linazidi kufukuta kuelekea mchakato wa kupata jina la mgombea kutokana na tabia ya baadhi ya viongozi kupigia debe majina na watu wanaoamini wakishinda watanufaika nao kwa kulinda masilahi binafsi.
 
Akizungumza na Mpekuzi  jana, kwa sharti la kutoandikwa jina, mmoja wa makada maarufu wa chama hicho ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ( NEC-CCM), alisema kuna mgawanyiko mkubwa miongoni mwa vigogo wa chama hicho katika kupata jina na mgombea urais hali ambayo alisema ina kila dalili za kusambaratisha chama hicho.
 
“Kuna tatizo katika kupata jina, tena ni tatizo kubwa, tatizo hili lipo kwa baadhi ya viongozi wa chama chetu kila mmoja anatembea na jina la mtu wake mfukoni. Wanahangaika kujipitisha huku na kule kwa visingizio mbalimbali huku mkono mwingine wanapitisha ajenda za kunadi watu wao.
 
Hatutakubaliana na hili! Wana-CCM waachwe waamue! Sio kuleteana majina kwa ujanja ujanja hapa,” alilalamika kada huyo na kuongeza; 
 
"Hata Pinda (Waziri Mizengo Pinda) juzi akiwa Iringa, ameonya tabia ya viongozi kutaka kuwachaguliwa wananchi viongozi...Pinda hakutoa kauli hiyo hewani, bali anajua kinachofanyika."
 
Alionya kwamba mitazamo tofauti ya vigogo hao kubeba watu wao imesababisha mpasuko mkubwa ndani ya chama na ili kuokoa hilo, busara kubwa inahitajika.
 
"Wanafikiri hatujui, kila mmoja ana mtu wake wanahangaika usiku na mchana, sisi tunawasubiri wakifanya kosa katika hili wataona matokeo yake, CCM itameguka vipande vipande.
 
Kwa tabia hii, wallah CCM inahesabu siku!” Alidai kada huyo na kuongeza;
 
“Tunaambiwa baadhi ya vigogo walibeba hadi majina ya baadhi ya waliotimuliwa kwenye Escrow. Wakahaha sana kupima upepo na kunadi kiujanja ujanja, eti wawe wagombea wa chama. Haya mambo, sielewi chama chetu kinakwenda wapi?
 
"Tunafika mahali watu wamejengeka hofu isiyokuwa na maana, wanachukia na kuogopa wengine bila sababu endapo watashika madaraka,” alisema.
 
Alifafanua zaidi kwamba tatizo lingine kubwa linalotishia kuathiri mchakato huo ni kile alichoita, hofu ya ovyo ya baadhi ya vigogo, kuogopa watu fulani wakishika madaraka.
 
“Leo hii watu wanashindwa kutenda haki kwa kuhofia masilahi yao. Wanalazimisha kubeba hata wasiobebeka. Nini hii? Kupata mgombea wa chama si jukumu la kifamilia au kikundi fulani! Hii si kazi ya familia moja ama mbili, hapana! 
 
"Mgombea asipatikane kwa kupendezesha au kulinda masilahi ya watu. Tunatafuta mgombea ambaye Mungu akimvusha anakuwa rais wa Watanzania wote. 
 
"Tukichanganya mambo, kwa suala zito kama hili kwa maslahi binafsi, majibu yake tutapata muda si mrefu, chama kitaumbuka na wengine hatupo tayari kuumbuka kwa hofu za watu binafsi zisizo na tija kwa chama na taifa kwa ujumla. Tumekitoa mbali chama hiki,” alionya.
 
Alisema CCM ina viongozi wengi wazuri wenye upeo usiotiliwa shaka, hivyo hakuna sababu ya kumhofia yeyote kwani chama kinatafuta kiongozi wa chama na Watanzania wote na siyo korokoroni wa kulinda familia moja au kaya.
 
Kada huyo alisisitiza kuwa kila mwana-CCM ana haki ya kugombea nafasi yoyote ndani ya chama bila hofu wala vitisho na wanachama ndio wenye jukumu la kumkubali au kumkataa kwa misingi ya kidemokrasia.
 
Alishauri vikao vyote vya maamuzi ndani ya chama kutenda haki na kupitisha mtu kwa sifa, uwezo rekodi na maadili yake katika kuwatumikia wananchi.
 
Alisisitiza kuwa shughuli ya kupitisha jina la mgombea wa CCM inapaswa kufanywa kwa tahadhari kubwa na kuomba viongozi wakongwe wa chama hicho wakiwemo Mzee Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, John Malecela, Pius Msekwa na Aman Karume kusaidia kubaini, kushawishi na baadaye kupitisha majina ya watu wanaofaa kubeba jukumu hilo.
 
“Mimi nashauri tena kwa msisitizo, viongozi watakaosimamia mchakato huu watende haki. Wafuate kanuni, wazingatie sifa 13 za mgombea urais. Kwa hili kuna mtu sitaki kumnyima haki yake, lazima nimsifu , huyu ni Comredy Mangula (Philip-Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara ).
 
"Kwa kusimamia haya Mangula ni jasiri na mkweli hana kona kona za kubeba mtu au watu, wakati baadhi wana majina mifukoni yeye ana sifa na vigezo mfukoni mwake.”
 
Kada huyo alishauri wana-CCM wenye sifa kujitokeza bila woga kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo urais muda utakapofika. Alisisitiza kuwa haki pekee ndiyo itasaidia kupata mgombea bora anayekubalika na wanachama na Watanzania wote.

No comments: