Jumuiya ya Serikali za Mitaa (ALAT) Shinyanga Yatangaza Kumuunga Mkono Edward Lowassa - LEKULE

Breaking

23 Feb 2015

Jumuiya ya Serikali za Mitaa (ALAT) Shinyanga Yatangaza Kumuunga Mkono Edward Lowassa


Vuguvugu la kumuomba kugombea urais aliyekuwa waziri mkuu wa Tanzania, Edward Lowassa, linaendelea kupamba moto baada ya wenyeviti wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa nchini (ALAT) mkoani Shinyanga kumtaka atangaze rasmi nia ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 
Akitoa ombi hilo mbele ya waandishi wa habari juzi mjini Shinyanga kwa niaba ya wenyeviti wenzake wa halmashauri za wilaya mkoani humo, Mwenyekiti wa ALAT mkoani Shinyanga, Justin Sheka, alisema wanaamini mtu anayestahili kupokea kijiti cha urais, Rais Jakaya Kikwete si mwingine bali ni Lowassa.
 
Sheka, alisema yeye na wenyeviti wenzake wa Halmashauri za wilaya mkoani Shinyanga wanaamini iwapo Lowassa atamrithi Rais Kikwete, ataweza kuendeleza mipango yote ya maendeleo itakayoachwa na rais anayemaliza muda wake na kwamba wanaompinga asigombee urais hawaitakii mema nchi yao.
 
Alisema ni wakati mwafaka hivi sasa kwa wana-CCM wote wanaotoka mikoa ya Kanda ya Ziwa waliotangaza nia au kutaka kutangaza kugombea nafasi ya urais waunganishe nguvu zao kwa Lowassa ambaye ndiye mwenye uwezo wa kufanya mambo makubwa kutokana na ujasiri alionao wa kuchukua maamuzi magumu kila panapostahili.
 
“Sisi tunaamini mtu ambaye anastahili kuvaa viatu vya Rais Kikwete kwa hivi sasa ni Lowassa, waswahili walisema, Mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni, huyu bwana pamoja na mapungufu ya hapa na pale ya kibinadamu, lakini bado ndiye mwenye uwezo mkubwa wa kuitumikia nchi hii akilinganishwa na wengine,” alisema.
 
“Uzoefu wa Lowassa unafahamika na Watanzania wengi hasa wale wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, yapo mambo mengi aliyoyafanya akiwa waziri mkuu hasa katika sekta ya elimu, kabla ya mwaka 2007, hatukuwa na sekondari nyingi, lakini baada ya kauli yake ya ujenzi wa sekondari za kata tumepata shule nyingi za kutosha,” alieleza Sheka.
 
Sheka ambaye pia ni mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, alisema wapo baadhi ya Watanzania wanaopinga na kudai Lowassa hastahili kukabidhiwa urais wa nchi hii kwa vile tu wanachuki binafsi dhidi yake au hawaitakii mema Tanzania.
 
“Sisi tumekaa na kutafakari sana huku tukiwachambua wana CCM wote ambao tayari wametangaza nia ya kutaka kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika nchini kote Oktoba 25, mwaka huu, tumebaini kati yao mtu mwenye uzoefu na uwezo mkubwa ni Lowassa,” 
  
“Hatusemi wengine hawafai, lakini tunafikiri suala la uzoefu wa kutosha wa kiuongozi ni jambo muhimu, pia mgombea lazima awe na sifa ya ziada tunataka rais ajaye awe ni yule mwenye uwezo wa kufanya maamuzi magumu pale inapohitajika kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wake, na mtu huyo si mwingine bali Lowassa,”
 
“Kwa upande wetu wenyeviti wa ALAT kutoka halmashauri za wilaya mkoani Shinyanga tunamuomba mheshimiwa Lowassa ambaye mpaka sasa hatujasikia kauli yake rasmi atamke wazi kwamba atagombea urais na sisi tuko nyuma yake tutamuunga mkono kwa nguvu zote,” alieleza Sheka.
 
“Binafsi naamini wana CCM wote waliotangaza nia wanafaa, lakini lazima tuangalie miongoni mwao ni mtu gani mwenye uzoefu mkubwa wa kiuongozi hasa upande wa utawala, mwenye maamuzi ya papo kwa papo kwa masilahi ya taifa lake, na hawa wengi wanaweza kupewa nyadhifa nyingine ili kuunda serikali imara,” alisema Sheka.

No comments: