SHIRIKA LA EQUALITY FOR GROWTH (EfG) LA ZINDUA MRADI WA MSAADA WA KISHERIA KWA WAFANYABIASHARA - LEKULE

Breaking

14 Feb 2015

SHIRIKA LA EQUALITY FOR GROWTH (EfG) LA ZINDUA MRADI WA MSAADA WA KISHERIA KWA WAFANYABIASHARA

Kaimu Mkurugenzi wa Halmshauri ya Wilaya ya Lushoto, Dk.Hassan Shelukindo (katikati), akikata utepe kuashiria uzinduzi wa  mradi wa msaada wa kisheria kwa wafanyabiashara sokoni na ofisi ya mradi huo wilayani Lushoto mkoani Tanga jana. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la  Equality for Growth (EfG), Jane Magigita na Katibu Tawala wa wilaya hiyo (DAS), Josephine Kisigila. Mradi huo unaendeshwa na EfG.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la  Equality for Growth (EfG), Jane Magigita akitoa hutuba fupi kwa mgeni rasmi.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmshauri ya Wilaya ya Lushoto, Dk.Hassan Shelukindo akizungumza katika hafla hiyo.













WAJASIRIAMALI wanawake wametakiwa kutumia mafunzo ya usimamizi wa sheria katika masoko waliyopata kwa kuwaelimisha wengine badala ya kukaa nyumbani bila ya kutoa elimu hiyo.

Mwito huo ulitolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmshauri ya Wilaya ya Lushoto Dk.Hassan Shelukindo wakati wa uzinduzi wa ofisi ya mradi wa msaada wa kisheria kwa wafanyabiashara sokoni na ofisi ya mradi huo wilayani humo  mkoani Tanga jana kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmshauri hiyo Jumanne Shauri. 

"Ninyi Wanawake wa Lushoto mmepata bahati kubwa ya kuletewa mradi huu pamoja na mafunzo haya mliyopata nawaombeni nendeni mkayafanyie kazi katika maeneo yenu" alisema Dk. Shelukindo

Alisema elimu waliyoipata ya msaada wa kisheria ni muhimu sana kusaidia jamii katika masoko na itasaidia kupunguza unyanyasaji wa kijisinsia.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la  Equality for Growth (EfG), ambalo linaendesha mradi huo, Jane Magigita alisema lengo la mradi huo katika wilaya hiyo ni kuhamasisha na kulinda haki za wafanyabiashara iwanawake katika masoko kwa kuwapatia elimu ya sheria, biashara, elimu ya vicoba, elimu ya uongozi na usimamizi wa vikundi.

Alisema EfG ni shirika la pekee nchini linalotoa msaada wa kisheria kwa sekta isiyorasmi hivyo kuonesha ni kiasi gani sekta hiyo ilivyo sahulika.

Alisema EfG  inaendesha mradi huo katika masoko ya wilaya ya Lushoto pamoja na vikundi mbalimbali vya maendeleo na kuwa shirika hilo linawajibika kutoa mafunzo  ya siku 25 kwa wasaidizi 25 ambao watasambaza huduma sheria kwa jamii.

Alisema mafunzo hayo yanatolewa kwa awamu tano ambapo kila awamu yatakuwa yanafanyika kwa  takribani siku tano.

" Shirika linawajibika kutoa mafunzo mafunzo mbalimbali kwa wafanyabiashara ikiwa na lengo la kuinua hali za wanawake wafanyabiashara sokoni kupitia mafunzo ya biashara, uundwaji wa vikundi vya Vicoba, mafunzo mbalimbali kwa watendaji na viongozi wa Halmshauri ya wilaya ya Lushoto kwa lengo la kuboresha hali za wafanyabiashara sokoni" alisema Magigita.

Alisema mpaka sasa shirika hilo limefanikiwa kuwapatia mafunzo ya sheria ya siku tano wasaidizi wa sheria 25, wanaume 8 na wanawake 17 kutoka katika masoko na wengine kutoka katika vikundi vya maendeleo ndani ya Halmshauri ya Wilaya ya Lushoto.

Alisema pia wanakituo maalumu cha msaada wa sheria katika ofisi za EfG Lushoto ambapo wafanyabiashara mbalimbali wanaruhusiwa kupeleka matatizo yao ya kisheria kila siku za Jumatatu na Jumatano kuanzia saa tatu asubuhi mpaka saa 10 jioni.




No comments: