BAADHI ya vifaa vya abiria vilivyoporwa katika tukio la utekaji wa magari 11 uliofanywa na majambazi waliokuwa na silaha za jadi mkoani Manyara mwanzoni mwa wiki hii, vimekutwa vikizagaa katika maeneo yalikofanyika uporaji huo.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa polisi mkoani Manyara, Christopher Fuime alisema vitu vilivyopatikana ni pamoja na laini za simu 14 na simu zinazouzwa kwa bei ndogo na kwamba jeshi hilo linaendelea kuwasaka majambazi hao ili kuwachukulia hatua.
Kamanda Fuime alisema katika tukio hilo majambazi zaidi ya wanane wakiwa na silaha za jadi waliteka magari 11 katika kijiji cha Gehandu kilichopo katika barabara kuu ya Babati–Singida na kupora vitu mbalimbali kwa watu waliokuwa ndani ya magari hayo zikiwemo fedha taslimu na simu za mkononi.
Alifafanua kuwa katika tukio hilo kiwango cha juu cha fedha zilizoporwa ni Sh 600,000 na kwamba hakuna mtu aliyejeruhiwa kwa kuwa majambazi hao walipoona idadi ya magari yanazidi kuongezeka na kufikia 18 katika eneo walipoweka vizuizi waliamua kukimbia kusikojulikana.
No comments:
Post a Comment