Bangi kavu ya kilo 50 yawatupa jela miaka 15 - LEKULE

Breaking

22 Feb 2015

Bangi kavu ya kilo 50 yawatupa jela miaka 15


Mahakama ya wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa imewahukumu raia watatu kutoka Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwenda jela miaka 15 au kulipa faini ya Sh milioni tatu kwa wote baada ya kutiwa hatiani kwa kukutwa na gunia mbili za bangi kavu yenye uzito wa kilo 50.
 
Washtakiwa hao Kasangu Paul (40), Mkambala Mwabu (39) na Kiwele Msaka (32) wote kutoka katika Mji wa Moba nchini DRC wameanza kutumikia kifungo cha miaka 15 kila mmoja baada ya kushindwa kulipa faini hiyo.
 
Akitoa hukumu hiyo mwishoni mwa wiki, Hakimu wa mahakama hiyo, Adamu Mwanjokolo alieleza kuridhika kwake na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.
 
“Nimetoa adhabu hii kali ili iwe fundisho kwa wengine ambao wana tabia kama yenu kila mmoja wenu atatumikia kifungo cha miaka mitano jela au kulipa faini ya Sh milioni moja,” alisema hayo alipokuwa akitoa hukumu.
 
Awali Mwendesha Mashtaka, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Hamimu Gwelo alieleza mahakamani hapo kuwa washtakiwa wote watatu kwa pamoja walitenda kosa hilo Februari 10 mwaka huu saa 2:00 usiku katika kijiji cha Korongwe mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Nkasi.
 
Aliongeza kuwa usiku huo wa tukio washtakiwa hao walikamatwa kijijini humo wakiwa katika harakati ya kumtafuta mnunuzi wa bangi hiyo.

No comments: