Watoto wanne wa familia moja wakazi wa kijiji cha kibambila wilayani Kakonko mkoani Kigoma wamefariki dunia na mmoja amelazwa katika kituo cha afya Kakonko baada ya kula chakula kinachosadikiwa kuwa na sumu.
Mganga mkuu wa wilaya ya Kakonko Dkt. Fadhil Seleman amewataja watoto hao waliofikishwa kituo cha afya Kakonko kuwa ni Neema Joseph, Jonas Joseph, Majaliwa Joseph, Yusuph Joseph wote wakiwa na umri wa kati ya miaka 11 na 18 walifikishwa hospitalini hapo wakiwa na hali mbaya na walipoteza maisha wakati wanaendelea kupatiwa huduma. Amesema kwamba uchunguzi wa awali umeonesha kuwa watu hao wamekula sumu katika chakula cha ugali.
Akizungumzia tukio hilo baba wa watoto hao Joseph Kajolo ambaye alinusurika katika tukio hilo amesema hajui chanzo cha tukio hilo huku baadhi ya wananchi wa Kakonko wameeleza kusikitishwa kwao na tukio hilo na kwamba vifo vya sumu katika wilaya hiyo vimekuwa vikijirudia mara kwa mara
Mkuu wa wilaya ya Kakonko Peter Toyima amesema polisi inamshikilia mtu mmoja kuhusiana na tukio hilo huku akiwataka wananchi kuacha vitendo vya kuwekeana sumu
No comments:
Post a Comment