Marekani itatuma wanajeshi zaidi kwenye kampeni dhidi ya kundi la Dola
la Kiislamu, huku jitihada za kimataifa dhidi ya kundi hilo zikiendelea.
Ufaransa imesema vijana wengi wanajiunga kwenye makundi ya siasa kali
Marekani inapanga kuwatuma wanajeshi wengine 1,500 kwenda kutoa mafunzo na ushauri kwa wanajeshi wa Iraq katika vita dhidi ya IS. Wizara ya ulinzi imesema wanajeshi hao wapya watapelekwa Iraq katika wiki chache zijazo bila kusubiri idhini ya bunge ya kuufadhili ujumbe huo.
Maafisa awali walidokeza kuwa waliwahitaji wabunge kuidhinisha ufadhili kabla ya wizara ya ulinzi kuanzisha operesheni hiyo, lakini Jenerali Lloyd Austin, mkuu wa majeshi ya Marekani katika Mashariki ya Kati, akapendekeza kuanzisha mpango huo kwa kutumia raslimali ambazo tayari anazo.
Makamu wa Rais Joe Biden leo atakuwa kiongozi wa karibuni kabisa wa Marekani wanaojaribu kuishinikiza Uturuki kuchukua jukumu lake katika kampeni ya muungano wa kimataifa dhidi ya wanamgambo wa IS. Ziara ya Biden inakuja baada ya wiki kadhaa za majibizano ya hadharani baina ya washirika hao wawili wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO.
Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Dovutoglu na mwenzake wa Iraq Haider al-Abadi
Rais wa Uturuki anasisitiza kuwa kama Marekani inataka msaada wake, lazima izingatie zaidi namna ya kumwondoa madarakani rais wa Syria Bashar al-Assad na wala siyo kupambana na IS tu. Recip Tayyip Erdogan anataka pawekwe eneo la usalama la kijeshi kaskazini mwa Syria ili kuwapa wapiganaji wa msimamo wa wastani nafasi ya kujiimarisha na kufanya mashambulizi dhidi ya Assad. Nayo Marekani inasisitiza kuwa haitaki kuingia vitani dhidi ya Assad ikisema haiwezekani kuwekwa amri ya kutoruka ndege dhidi ya jeshi la Syria. Kwingineko, Rais wa Syria Bashar al-Assad amesema “ushirikiano wa kimataifa” unahitajika ili kuliangamiza kundi la Dola la Kiislamu. Assad amesema kanda nzima inakabiliwa na kitisho cha wapiganaji hao wa jihadi ambao anahoji kuwa waliibuka kutokana na matunda ya sera mbovu na za uchokozi zilizowekwa na wale walioanzisha vita dhidi ya Syria.
Katika hatua nyingine Iraq na Uturuki zimekubaliana kuwa na ushirikiano wa karibu wa usalama na ujasusi kutokana na kitisho kilichopo kutoka kwa kundi la IS. Davutoglu amepinga madai kuwa nchi yake iliwezesha kusafirishwa kwa wanamgambo kupitia mipaka yake na kuingia nchini Syria. Alisema Uturuki hupokea watalii milioni 35 kila mwaka na haiwezi kuwazuia watu kuingia nchini humo, isipokuwa kama wana kesi dhidi yao.
Mjini Paris, ofisi ya mwendesha mashtaka imesema wapelelezi wameanzisha rasmi uchunguzi wa ugaidi dhidi ya raia watatu wa Ufaransa waliopewa mafunzo ya itikadi kali za kiislamu waliotoa wito kupitia video ya propaganda wa kufanywa mashambulizi nchini Ufaransa. Watu hao watatu wanatoa wito kwa Wafaransa kuungana nao vitani au wafanye mashambulizi ndani ya nchi yao.
No comments:
Post a Comment