RAIS Dk. John Magufuli amemtumbua mfanyabiashara mmoja maarufu Dar es Salaam, aliyebainika kufanya miamala ya fedha ya Sh milioni saba hadi nane kwa kila baada ya dakika moja.
Kutokana
na hesabu ya Sh milioni saba anayoingiza kwa dakika moja,
mfanyabiashara huyo hutengeneza Sh milioni 420 kwa kila saa moja, sawa
na Sh bilioni 5.2 kwa saa 12 na Sh trilioni 16 kwa mwezi ambazo halipi
Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
Rais
Magufuli amesema mfanyabiashara huyo aliyebainika kuwa na makampuni
mengi, alikuwa akishirikiana na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni
nchini (BRELA) pamoja na Mamlaka ya ato Tanzania (TRA).
Mkuu
huyo wa nchi alitoa kauli hiyo Ikulu, Dar es Salaam jana, baada ya
kuwaapisha wakuu wapya wa mikoa watatu katika hafla iliyohudhuriwa pia
na wakuu wa wilaya wateule.
Alisema waligundua jipu hilo baada ya kufuatilia kwenye mapato.
“Tulikuwa
tunafuatilia kwenye ‘revenue’ (mapato), kwenye zile VAT ambazo
zinatumika ‘ku-collect revenue’ (kukusanya mapato), yupo mtu mmoja
ambaye alikuwa ametengeneza kampuni zake nyingi, alikuwa anafanya
‘transaction’ (miamala) ya fedha kila dakika moja kati ya Sh milioni
saba na nane.
“Na
hizo risiti alikuwa anaziuza kwa wafanyabiashara wengine, kwenye VAT
anatakiwa kulipia kwa asilimia 18. Wafanyabiashara wengine hao walikuwa
wanauziwa kwa asilimia tano na wakishauza bidhaa wanakwenda kuomba TRA
iwarudishie hiyo asilimia 18, kwa hiyo Serikali imekuwa ikipoteza
asilimia 18.5, ni matrilioni na matrilioni ‘of money’ (ya fedha).
“Bahati
nzuri huyo mtu yuko kwenye mikono salama, tunafuatilia namna
tutakavyorudisha hizo fedha, na huyo mtu alikuwa ana-connection kati ya
watu wa BRELA na TRA… hiyo ndiyo Tanzania.
“Najaribu
tu kutoa mfano ili katika maeneo yenu mkasimamie mapato ya Serikali,
kwa sababu tumepoteza mapato mengi kuliko tunavyofikiria, huku
Watanzania wakiteseka sana, na mambo yanayofanyika ni ya ajabu,” alisema Rais Magufuli akiwaambia wakuu hao wa mikoa na wilaya.
Pamoja
na mambo mengine, Rais Magufuli alisema mchakato wa kupata wakuu wapya
wa wilaya ulikuwa mgumu, na kwamba amewaacha wengi wa zamani kwa kuwa
hawakutimiza vigezo alivyovitaka.
“Mchakato
wa kupata ma-DC ulikuwa mgumu kwa sababu ilibidi tuangalie historia ya
kila mmoja. Tuliangalia mambo mengi sana, lakini pia tuliangalia kwa
ku-preview atatimiza haya tunayotaka kuyafanya kwa miaka mitano?
“Na
ndiyo maana mnavyoona ma-DC wa zamani waliorudi ni 39, kwa hiyo wale
101 wote hawakurudi… niseme tu ukweli kwamba hawakufikia vigezo
tulivyokuwa tunavitaka,” alisema Rais Magufuli.
Alisema katika uteuzi huo, alichukua wakurugenzi kwa kuwa walifanya vizuri katika maeneo yao waliyokuwa wakiyaongoza.
“Tulichukua
wakurugenzi walio-perform vizuri katika maeneo yao. Wapya wako
takribani 100 na waliobaki ni hao kati ya 38 na 39. Ni matumaini yangu
kwamba mtakwenda kufanya kazi na kutimiza wajibu wenu.
“DC
ni nafasi kubwa ya uongozi katika Serikali na ndiyo maana mfano mkubwa
wa DC mstaafu ni Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa), ni kwa sababu alitimiza
wajibu wake na leo yuko hapa,” alisema.
Mkuu huyo wa nchi aliwapa mikakati ya kufanya kazi wakuu hao wa wilaya kwa kutimiza dhana ya kuchapa kazi kwa niaba ya Serikali.
“Nina
matumaini makubwa mtakwenda kutimiza dhana ya kuchapa kazi kwa niaba ya
Serikali, ninyi ndio wawakilishi wetu na ndio mnawakilisha wananchi wa
maisha yote.
“Watanzania
wana matatizo na changamoto kubwa. Ni matumaini yangu kwamba
hamtaniangusha na hamtaiangusha Serikali. Nina imani mtakwenda kutatua
matatizo ya wananchi, hasa walio masikini, sitegemei wala sifikirii
kwamba mkawe chanzo cha kutengeneza matatizo,” alisema Rais Magufuli.
Kutokana
na hali hiyo, aliwataka wasimamie haki, huku wakimtanguliza Mungu
katika kufanya kazi, kusimamia maadili, kutenda haki, kutojihusisha na
rushwa, kuwatumikia Watanzania bila kubagua dini, kabila wala vyama
vyao.
“Kikubwa
mkasimamie yale tuliyoyaahidi sisi wanaCCM, kwa sababu wakati
tunazunguka tukiomba kura, yapo tuliyoyaahidi, hayo mkayatekeleze kwa
nguvu zote.
“Na
wala asitokee mtu yeyote wa kuwakwamisha kutekeleza hayo, ninyi ndio
wakuu wa wilaya na ninyi watatu ndio wakuu wa mikoa. Mna mamlaka makubwa
ya kuweka mahabusu mtu masaa 48 halafu kesho yake ukamwachia. Ila
msiende kuonea watu, mkachape kazi.
“Imani
tuliyoionyesha kwenu sisi viongozi wenu mkaionyeshe kwa Watanzania
mnaowaongoza, mkashirikiane na viongozi mtakaowaongoza, wanasema umoja
ni nguvu, utengano ni udhaifu.
“Nina
uhakika mkisimama vizuri kwa kuzingatia maadili mliyonayo, na bahati
nzuri wengi mna uzoefu katika maeneo yenu. Mkawahamasishe Watanzania
katika wilaya na mikoa yenu kufanya kazi. Watanzania wengi tumezoea
kulalamika, tunataka tupewe, lakini hatufanyi kazi. Tukawasimamie
kuchapa kazi,” alisema.
Aliwataka
wakuu hao wa wilaya ambao pia ni wenyeviti wa kamati ya ulinzi na
usalama, kukemea rushwa katika maeneo yao na kusimamia mapato ya
Serikali.
“Huwa
inatokea saa nyingine wakurugenzi kwa sababu kuna fedha nyingi
tunapelekaga kule, wanadhani ni zao wakati ni za Serikali, mkawasimamie
bila woga.
“Kupitia halmashauri zenu, mkahakikishe fedha hizo zinatumika kulingana na matakwa ya kanuni na sheria za nchi,” alisema Rais Magufuli.
No comments:
Post a Comment