Askari wa Burundi wakipiga doria katika mitaa ya Bujumbura, baada ya shambulio la guruneti, Februari 3, 2016.
Mapigano
makali yanaripotiwa tangu Alhamisi hii Asubuhi katika kijiji cha Mubuga
mtaa wa Gasanda, mkoani Bururi, kusini mwa Burundi. Mapigano hayo ni
kati ya vikosi vya usalama vikishirikiana na jeshi na kundi la waasi.
Mpaka
sasa hasara kufuatia mapigano hayo haijajulikana, lakini chanzo cha
polisi kinabaini kwamba mpiganaji mmoja ameuawa na watu wawili
wamejeruhiwa, huku wapiganaji watano wakikamatwa na silaha zao.
Kiongozi
wa vijana wakereketwa wa chama madarakani (Imbonerakure) na askari
polisi wamejeruhiwa kwa mujibu wa mkuu wa mkoa wa Bururi, Christian
Nkurunziza.
“Mapema
asubuhi tulipata taarifa kwamba kuna kundi la majambazi 11 wenye silaha
ambao walikua katika kijiji cha Mubuga, vikosi vya usalama viliwaona na
kuanza kupambana nao”, amesema mkuu wa mkoa wa Bururi, akihojiwa kwa
njia ya simu na RFI.
“Jambazi mmoja ameuawa na wengine watano wamekamatwa”, Christian Nkurunziza ameongeza.
Jambazi
au majambazi ni neno linalotumiwa mara kwa mara na serikali, ikimaanisha
wapiganaji wa makundi ya waasi yaliyoanzishwa baada ya maandamano dhidi
ya muhula wa tatu wa Rais Pierre Nkurunziza.
Kwa
mujibu wa shahidi ambaye hakutaka jina lake litajwe, “askari polisi
mmoja na kijana kutoka kundi la vijana wa chama madarakani (ambao Umoja
wa Mataifa unawaita wanamgambo) wamejeruhiwa”.
Mkuu wa
mkoa wa Bururi amebaini kuhusu kijana huyo kutoka kundi la vijana wa
chama tawala (Imbonerakure) kwamba “mtu aliyejeruhiwa ni raia wa kawaida
ambaye alikua aliitikia wito wa serikali wa kushirikiana na vikosi vya
usalama kwa kuwakamata majambazi hao.”
Baadhi ya
wakazi wa kijiji cha Mubuga wameyatoroka makazi yao na wengine wamesema
kuwa na hofu ya kuwa huenda mapigano hayo yakachukua muda mrefu.
Mapigano
hayo yanatokea wakati ambapo serikali ya Bujumbura imekua ikibaini
kwamba tayari imerejesha hali ya utulivu nchini kote.
Hata
hivyo hali ya usalama imeendelea kudorora katika maeneo mbalimbali ya
nchi hiyo, ambapo magruteni na mauaji ya kuvizia au visa vya ulipizaji
kisasi vimekua vikiripotiwa.
Machafuko
nchini Burundi yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 500, kwa mujibu wa
mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu na zaidi ya watu 270,000
kukimbilia nje ya nchi kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa
linalohudumia wakimbizi (UNHCR).RFI
No comments:
Post a Comment