Lesotho Yakubali Kutekeleza Masharti Ya SADC - LEKULE

Breaking

29 Jun 2016

Lesotho Yakubali Kutekeleza Masharti Ya SADC

WAZIRI MKUU wa Lesotho, Dk. Pakalitha Mosisili amekubali kutekeleza masharti yaliyowekwa na Wakuu wa Nchi na Serikali na Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Uchumi na Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC Double Troika Summit), na kuridhia timu ya uchunguzi kwenda nchini humo kufanya uchunguzi wa hali ya kiusalama na kisiasa.

Dk. Mosisili ametoa uamuzi huo leo (Jumanne, 28 Juni, 2016) wakati wa kikao maalum cha Wakuu wa Nchi na Serikali (SADC Summit) na wakuu wa nchi wanaounda Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama (SADC Organ on Politics, Defense and Security Cooperation) kilichofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa (GICC), jijini Gaborone, Botswana.

Pia amekubali viongozi waupinzani na baadhi ya maofisa wa kijeshi wanaoishi uhamishoni ambao walikimbia machafuko yaliyotokea nchini humo warejee nchini mwao na kuahidi kwamba atahakikisha wanapatiwa ulinziwa kutosha.

Januari mwaka huu, mkutano wa SADC Double Troika uliagizakwambaifikapo Februari Mosi, mwaka huuSerikali ya Lesotho iwe imetangaza matokeo ya Tume iliyoundwa kuchunguza matatizo ya kisiasa na kiusalama nchini humo hususan mazingira yaliyopelekea kifo cha marehemu Luteni Jenerali Maaparankoe Mahao ambaye alikuwa Mkuuwa Majeshi.

Kwaupande wake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye alikuwa akimwakilisha Rais Dk. John Pombe Magufuli katika kikao hicho amesema wamepitia ripoti iliyoundwa na timu ya SADC iliyochunguza kuhusu matatizo ya Lethoto ambayo iliwahoji Viongozi wa Serikali, Jeshi, Bunge na familia ya marehemu Luteni Jenerali Mahao.

“Lengo la hatuahiiza SADC ni kuhakikisha inarejesha hali ya amani na utulivu kwenye maeneo ya siasa, ulinzi na usalama katika nchi wanachama wa Jumuiya hiyo ili wananchi wake waweze kuishi vizuri,” amesema

Pia Waziri Mkuu amesema Tanzania inatarajiwa kukabidhiwa uenyekiti wa Wakuu wa Nchina Serikali na Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Uchumi na Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC Double Troika Summit), Agosti mwaka huu ambapo kitafanyika kikao kingine nchini  Tanzania.

Mkutano huo wa ulifunguliwa na Rais wa Botswana, Mhe. Lt. Jen. Seretse Khama Ian Khama na ulihudhuriwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye alikuwa akimwakilisha Rais Dk. John Pombe Magufuli;  Rais wa Afrika Kusini, Bw. Jacob Zuma; Rais wa Msumbiji, Bw. Filipe Jacinto Nyusi; Rais wa Zimbabwe, Bw. Robert Mugabe, Mfalme Muswati wa III wa Swazland.

SADC Double Troika ni kikao maalum kinachojumuisha Wakuu wa Nchi na Serikali (SADC Summit) na wakuu wa nchi wanaounda Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama (SADC Organ on Politics, Defense and Security Cooperation).

SADC Double Troika ni mkutano unaohusisha viongozi wakuu watatu wanaoongoza chombo cha ushirikiano wa siasa, ulinzi na usalama na wengine watatu kutoka kwenye Mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa SADC. Hawa wanawakilisha mwenyekiti aliyepo madarakani, mwenyekiti aliyemaliza muda wake na mwenyekiti ajaye ambaye huwa ni makamu mwenyekiti.

Chini ya muundo wa SADC, kuna mambo makuu mawili; la kwanza likiwa ni utangamano wa kikanda ambao unasimamiwa na mkutano wa wakuu wa nchi (SADC Summit) na la pili ni la siasa, ulinzi na usalama ambalo linasimamiwa na chombo maalum (SADC Organ).


Wajumbe wa mkutano wa SADC Organ ni Msumbiji (Mwenyekiti); Afrika Kusini (Mwenyekiti aliyemaliza muda wake) na Tanzania inayotarajia kuchukua uenyekiti wa chombo hiki ifikapo Agosti, 2016. Botswana, Zimbabwe na Swaziland ndizo zinaunda SADC Summit.

No comments: