MAREKEBISHO
ya Sheria mpya ya Manunuzi, yamewasilishwa bungeni yakitamka kufyeka
posho za watendaji, wanaosimamia mchakato wa zabuni na kuondoa vikao vya
bodi kutoka 12 kwa mwaka hadi vinne, ikisisitiza kuziba mianya ya
rushwa na kuongeza uwazi.
Aidha,
muswada wa marekebisho hayo, unataka kampuni au mshauri wa nje ili
apewe zabuni katika shughuli zinazogharimiwa na fedha za umma,
ahakikishe asilimia 60 ya wafanyakazi wa kampuni yake ni Watanzania.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, aliyasema hayo jana mjini Dodoma
wakati akiwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma
wa Mwaka 2016.
Kupungua
kwa vikao vya bodi, kumeelezwa na Dk Mpango kuwa kutapunguza gharama
zinazotokana na posho ya vikao vya bodi ya zabuni na ada zinazolipwa kwa
kamati zinazohusika na mchakato ya zabuni.
Aidha,
posho zinazotokana na utekelezaji wa majukumu ya kazi ya kila siku ya
washiriki itafutwa. Hata hivyo, imeruhusu kuwapo kwa vikao vya dharura
pale Mwenyekiti wa Bodi akiona ni lazima.
Pamoja
na kupunguzwa vikao, muda wa zabuni nao umepunguzwa na pia taasisi
nunuzi itaruhusiwa kufanya majadiliano ya bei wakati wa mchakato wa
zabuni kwa lengo la kupunguza bei ya ununuzi na kuongeza bei ya kuuza
mali za serikali.
Dk
Mpango alisema sheria hiyo mpya, itaziba mianya ya rushwa, kuongeza
kasi, uwazi, uwajibikaji na kuleta upendeleo maalumu kwa kampuni za
Tanzania katika zabuni za ndani na za kimataifa.
Pia sheria hiyo itaongeza ufanisi na kupata thamani halisi ya fedha, inayotumika kwa kununua huduma na bidhaa.
Dk
Mpango alisema pamoja na kuongeza uwajibikaji, sheria hiyo mpya
itapunguza vikao vya bodi hadi kuwa kimoja kwa robo mwaka na vikao vya
dharura, kufanyika pale ambapo mwenyekiti ataona inabidi.
Pamoja
na maelekezo hayo mapya, serikali pia itaanza kununua bidhaa na huduma
kwa bei inayoendana na bei ya soko, iwapo wabunge watapitisha
marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma.
Pamoja
na ununuzi wa bei ya soko, sheria mpya imelenga kuweka sharti la
kisheria kutoa upendeleo katika zabuni mbalimbali, hasa kwa makundi
maalumu kama vile wanawake, vijana, wazee na watu wenye mahitaji
maalumu.
Alieleza
kuwa sheria mpya imelenga kuiwezesha serikali, kunufaika na matumizi ya
viwango na kuweka sharti la kisheria la kutumia mifumo ya kuongeza
uwazi katika ununuzi ili kuongeza uadilifu na uwajibikaji.
Kwa
mujibu wa waziri, sheria mpya imelenga kurahisisha ununuzi wa umma na
kuipa faida serikali baada ya kuwapo kwa changamoto nyingi kwa Sheria
Namba 7 ya Mwaka 2011, ambayo ilianza kutekelezwa mwaka huo.
Changamoto
hizo ni pamoja na bei ya juu ya bidhaa na huduma zinazonunuliwa na
serikali kulinganisha na bei ya soko kutokana na zuio la majadiliano
kuhusu bei kati ya taasisi nunuzi na mzabuni.
Pamoja
na changamoto ya bei, kumekuwepo na muda mrefu wa mchakato, gharama
kubwa zinazotokana na matangazo na vikao mbalimbali vya kupitia zabuni,
kutozingatiwa kwa viwango na kutokuwepo kwa upendeleo katika ushiriki wa
zabuni kwa makundi maalumu.
Mapendekezo
ya muswada huo, pia yametaka pale kampuni au taasisi ya umma
inapolazimika kufanya ununuzi kutoka nje ya nchi, hasa kama ni suala la
ushauri linafanywa na kampuni ya nje ya nchi, ofisi hiyo ya serikali
inalazimika kuhakikisha kuna wataalamu wa ndani ya nchi.
Aidha,
kampuni au mshauri huyo wa nje ili apewe zabuni katika shughuli ambazo
zinagharimiwa na fedha za umma, kuna kigezo cha kuhakikisha wafanyakazi
wa kampuni yake, zaidi ya asilimia 60 ni Watanzania.
Mbali
na kuwa na asilimia 60 ya wafanyakazi Watanzania, kampuni husika lazima
ieleze kiwango cha bidhaa na huduma zinazozalishwa ndani ya nchi,
ambazo itazinunua katika utekelezaji wa shughuli zake.
Nayo
Kamati ya Bunge ya Bajeti imeitaka serikali kusimamia na kuhakikisha
kwamba watumishi wa umma ambao hawastahili kupewa magari, watumie magari
yao binafsi ; na wale ambao wanastahili wakopeshwe magari na serikali
na kupewa posho kidogo kwa ajili ya mafuta na matengenezo.
Pia, imeitaka serikali iandae utaratibu wa kununua magari kwa pamoja yasiyo na gharama kubwa kulingana na bei ya soko.
Akisoma
maoni ya Kamati ya Bunge ya Bajeti kuhusu Muswada wa Marekebisho ya
Sheria ya Ununuzi wa Umma wa mwaka 2016, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Hawa
Ghasia alisema kamati imekubaliana na serikali kufanya manunuzi kwa
kuzingatia thamani ya fedha kwa bidhaa, ikiwamo manunuzi ya magari
Alisema muswada huo unaonesha kwamba inawezekana kupunguza gharama za serikali kwa kufuata thamani ya fedha.
Aidha
kamati hiyo imeishauri serikali kuanzisha mfuko wa uwezeshaji wa
makandarasi ili waweze kumudu utoaji wa huduma mbalimbali, zinazohuisha
gharama kubwa, mfano ukandarasi wa barabara.
Mfuko huo utakuwa ukitoa dhamana. Pia kamati hiyo inataka kujua mwanzo wa matumizi ya sheria mpya.
Wabunge
waliochangia muswada huo, waliitaka serikali nayo kujiunga katika
sheria hiyo kwa kuona kwamba inawalipa wazabuni mapema au inaeleza
watakavyoweza kuwa wazabuni wanapochelewesha malipo, hasa kutokana na
kampeni yake ya ununuzi kwa bei ya soko.
Wabunge
hao walisema kwamba serikali inajua sababu za bei kubwa na hivyo inafaa
ikajipanga kuondoa kasoro hiyo ili hiyo sheria iweze kutekelezeka.
Mbunge
wa Mwibara, Kangi Ligora (CCM) alitoa tahadhari kwamba sheria
inabadilishwa Ibara 40 ambayo ni sehemu kubwa na kusema kwamba lazima
ijiandae kuondoa sababu za bei kubwa na pia kutofuta kipengele cha
kamati ya mipango na fedha kwenye halmashauri kupitia zabuni kwa lengo
la kujiridhisha.
Kauli ya kutofuta kipengele hicho katika muswada, pia ilizungumzwa na wabunge waliochangia jana.
Aidha
wengine walitaka kuwapo na dirisha kwa ajili ya dharura na hasa dirisha
kwa ajili ya bidhaa za afya na tiba. Wabunge wengine waliochangia ni
Martha Mlata, Rita Kabati, Ali Hassan, Dk Diodorus Kamara, Japhet
Asunga, Adadi Rajab, Jitu Son, John Kadutu na Amina Mollel.
No comments:
Post a Comment