Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limekifunga
kiwanda cha Mount Meru Millers Ltd kilichopo wilayani Bunda, mkoani
Mara na kukipiga faini ya Sh12 milioni kwa uharibifu wa mazingira
kinyume cha Sheria ya Kulinda na Kuhifadhi Mazingira.
Hatua hiyo
ya NEMC imekuja baada ya malalamiko ya muda mrefu kuhusu
kiwanda hicho kutiririsha maji yenye kemikali zenye sumu katika makazi
ya watu, vyanzo vya maji na kwenye mashamba ya mpunga.
Mratibu
wa NEMC Kanda ya Ziwa, Anna Mdamo alisema uchunguzi uliofanywa na baraza
hilo Machi 22, mwaka huu, ulibaini kuwa kiwanda hicho kinaendesha
shughuli zake kinyume cha Sheria ya Mazingira ikiwa ni pamoja na
kutokutumia mtambo wa kutibu maji kabla ya kuyaachia kuingia mitaani.
Mmoja
wa viongozi wa kiwanda hicho aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina alikiri kupokea barua ya kukifunga toka juzi.
Kwa
mujibu wa NEMC, kiwanda hicho kinatakiwa kulipa faini ndani ya siku 14,
vinginevyo hatua zaidi zitafuata ikiwamo kufikishwa mahakamani.
Mkuu
wa Idara ya Mazingira ya Halmashauri ya Mji wa Bunda, Majura Masumbuko
aliishukuru NEMC kwa kuchukua hatua dhidi ya kiwanda hicho
kilichosababisha mgogoro kati ya mamlaka za Serikali wilayani Bunda.
No comments:
Post a Comment