Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) ipo kwenye maandalizi ya kupunguza
wafanyakazi wasiohitajika kwa sasa kutokana na kasi ya mabadiliko ya
sayansi na teknolojia.
TTCL inayotoa huduma za simu na pia kutoa
mitandao kwa kampuni zilizo na leseni ya huduma hizo, itapunguza
wafanyakazi 400 ili kuongeza ufanisi na hivyo kumudu ushindani katika
sekta ya mawasiliano dhidi ya kampuni binafsi.
Mapema mwaka jana,
Serikali iliamua kununua asilimia 35 ya hisa za TTCL zinazoshikiliwa na
kampuni kubwa ya huduma za simu nchini India, Bharti Airtel na baadaye
mwezi Mei, 2015 aliyekuwa Naibu Waziri wa Sayansi na Mawasiliano,
January Makamba aliliambia Bunge kuwa Serikali iko katika maandalizi ya
mwisho ya kumiliki hisa zote za kampuni hiyo kubwa kwa huduma za simu za
mezani nchini.
Chanzo cha habari kutoka ndani ya kampuni hiyo
kinaeleza kuwa kati ya wafanyakazi 1,500 wa TTCL, zaidi ya 400
watapoteza ajira katika mpango huo wa kudhibiti gharama za uendeshaji.
“TTCL
itaomba fedha ili kuwalipa wafanyakazi zaidi ya 400 wanaotakiwa
kupunguzwa,” alisema mtoaji habari huyo .
“Kuna wafanyakazi wanaingia asubuhi na kutoka jioni
bila kufanya kazi yoyote ile na mwisho wa mwezi anakula mshahara zaidi
ya Sh800,000. Kumuachisha kazi inakuwa vigumu sana, lakini kama TTCL
itasaidiwa na Serikali kufanikisha hilo, itakuwa imejikwamua kwa kiwango
fulani.”
Hata hivyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Dk Kamugisha
Kazaura alisema maandalizi ya kupunguza wafanyakazi yataanza mwezi
Aprili kupitia ukaguzi maalumu wa rasilimali watu.
Alisema hatua ya
awali kwa sasa ni kuangalia mpango mkakati wa kampuni hiyo jinsi gani
inaweza kujijenga upya kutokana na changamoto ya ushindani wa
kibiashara.
“Kwa sasa siwezi kusema ni wafanyakazi wangapi
wanatakiwa kupunguzwa kutoka miongoni mwa 1,500 kwa kuwa kila mmoja
amekuwa akiwasilisha taarifa yake mwisho wa mwaka na wapo wanaotimiza na
wengine wanashindwa kutimiza malengo ya kampuni, mchango wao unakuwa
kidogo,” alisema.
Dk Kazaura alisema katika lengo la mpango huo
ni kuangalia jinsi gani watalaamu waliopo wanatumika kuendana na
mabadiliko ya teknolojia.
Alisema kuna wataalamu waliopo kwa
sasa ambao hutumika katika shughuli za uzalishaji, lakini kulingana na
mabadiliko ya kazi nyingi kufanywa na teknolojia mpya na nafasi ya kazi
nyingi katika taaluma zao zimepungua.
“Pamoja
na hivyo lakini
itakuwa vigumu kuwafahamu ni wangapi ambao hawazalishi katika kampuni
hadi kazi hiyo ya HR auditing (ukaguzi wa rasilimali watu)
itakapokamilika. Itakuwa tathmini itakayotoa mwelekeo mpya wa kampuni,” alisema.
Alipoulizwa
kuhusu mpango wa TTCL kuomba msaada serikalini, Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema hana taarifa
yoyote.
Hata hiyo, alisema TTCL ina mamlaka yake ya kujiamulia kuajiri au kupunguza wafanyakazi bila kuingiliwa na Serikali.
No comments:
Post a Comment