Waziri Mkuu Awapongeza Lulu na Richie kwa Kunyakua Tuzo - LEKULE

Breaking

11 Mar 2016

Waziri Mkuu Awapongeza Lulu na Richie kwa Kunyakua Tuzo

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa  amesema Serikali imefarijaka kwa ushindi wa wasanii wa filamu nchini walioshinda tuzo za  filamu Afrika za mwaka 2016(African Magic Viewers Choice Award) ziliyofanyika jijini Lagos nchini Nigeria mwishoni wa wiki iliyopita.

Waziri Mkuu Majaliwa, amesema hayo leo katika ukumbi wa mikutano ulipo katika  Ofisi yake  Jijini Dares Salaam, alipokutana na washindi wa tuzo za  filamu Afrika za mwaka 2016 (AMVCA)  ambao ni  Elizabeth Michael ‘Lulu’ aliyeshinda tuzo ya Filamu Bora ya Afrika Mashariki na Single  Mtambalike ‘Richie’ aliyeshinda tuzo ya Filamu Bora ya Kiswahili pamoja Naibu Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo, Mhe. Annastazia Wambura,Katibu Mkuu wa wizara Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Bi Joyce Fisso na wasanii wa filamu.

 “Serikali imefarijika sana kwa nyie kwenda Nigeria na kushinda na mmetumia lugha ya Kiswahili, lazima tutumie nafasi hii kuwatangaza  pia  mmuendelee na fani hii ili kuvutia wengi zaidi” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Aidha, Waziri Mkuu amewapongeza wasanii hao na kusema kuwa  Serikali itaendelea kushirikiana  na wasanii wakati wowote na amewataka kujipanga vizuri kutumia vyama vyao vya sanaa na kusisitiza kuwa  Mhe.  Rais John Pombe Magufuli ametoa matamko kadhaa  kuhusu sanaa  na wasanii  na ameendelea kushughulikia malalamiko yao ikiwemo suala la COSOTA, na kusema kuwa  baada ya taratibu zote kukamilika  suala hilo litasimamiwa na Wizara inayohusika na kazi za Sanaa.

Waziri Mkuu Majaliwa, pia amewataka watanzania kuacha tabia ya kutojiamini  na kujidharau, na kuwataka watu waige mfano kwa wasanii hao, na kuwashauri wasanii wote kwa ujumla kutumia vyombo vya habari kujiimarisha na kujitangaza.

Kwa  upande wao, wasanii waliopata  tuzo hizo kwa filamu ya “mapenzi ya Mungu” ya  Elizabeth Michael na filamu ya “Kitendawili” ya Single  Mtambalike, wameishukuru Serikali  kwa kuwathamini na kuonesha  ushirikiano katika kazi zao za sanaa, na wameahidi kuendelea  kutengeneza  kazi nzuri za sanaa ili ziweze kuitangaza Tanzania kimataifa.

Naye, Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania(TAFF) Saimon Mwakifamba ameishukuru Serikali kwa jitihada mbalimbali  inazofanya katika kusaidia tasnia ya sanaa kwa ujumla na ameahidi kuendelea kushirikiana na  Serikali katika kuendeleza tasnia hiyo kimataifa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea Tuzo kutoka kwa Msanii wa filamu Elizabeth Michael ambayo msanii huyo alishinda nchini Nigearia. Tukio hilo lilifanyika Ofisini kwa Waziri Mkuu jijini Dar es salaam Machi 11, 2016.

Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa akipokea tuzo kutoka kwa msanii wa filamu, Single Mtambalike ambayo msanii huyo alishinda nchini Nigeria. Tukio hilo lilifanyika Ofisini kwa Waziri Mkuu jijini Dar es salaam Machi 11, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) 

No comments: