Mchezaji wa timu ya Azam FC Shomary Kapombe jana amekabidhiwa shilingi Milioni 1/ kutokana na kutajwa kuwa mchezaji bora wa mwezi January 2016 kwenye ligi ya soka ya VPL inayoendelea ambapo amekabidhiwa kitita hicho kutoka kwa mdhamini wa ligi hiyo Vodacom Tanzania katika uwanja wa klabu anayoichezea Chamanzi Dar es Salaam.
Baada ya kuchukua mkwanja wake Kapombe amesema amefurahia kuwa miongoni mwa wachezaji waliopata tuzo na imezidi kumtia moyo na bidii ya kujituma zaidi >>> ‘Nashukuru Vodacom kwa kuwapatia zawadi wachezaji wanaofanya vizuri kwa kuwa inawazidishia kasi ya kujituma zaidi, pia nawashukuru wachezaji wenzangu wote wa Azam maana bila jitihada za pamoja sio rahisi mchezaji mmoja ukaibuka na kuonekana bora kwa kuwa katika mchezo wa soka sote tunategemeana’
Kwa upande wake Meneja Uhusiano wa Vodacom Tanzania Matina Nkurlu aliyeambatana na Ofisa wa Bodi ya Ligi Joel Balisidya pamoja na ofisa udhamini na matukio wa kampuni hiyo, Ibrahim Kaude katika kumkabidhi zawadi hiyo alimpongeza mchezaji huyo na kuongeza kusema kuwa Vodacom inajivunia mafanikio yanayoendelea kupatikana katika ligi hiyo na ina mpango wa kushirikiana na wadau wengine wa soka kuzidi kuiboresha zaidi.
Kapombe alitwaa tuzo mwezi January 2016 uliokuwa na raundi tatu na alicheza dakika zote 180 za mechi mbili za timu yake dhidi ya African Sports na Mgambo Shooting, mechi ya tatu ya Azam FC katika raundi hiyo dhidi ya Tanzania Prisons ilikuwa kiporo, na ilichezwa Februari 24, 2016.
Kapombe alifunga magoli yote mawili kwenye ushindi wa mabao 2-1 wa timu yake dhidi ya Mgambo Shooting. Pia alisaidia kupatikana bao la Azam kwenye mechi dhidi ya African Sports iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1, na mara nyingi mashambulizi ya timu yake yalianzia upande wake.
No comments:
Post a Comment