SSRA Yatetea Uraia Wa Dr Wangwe Ambaye Aliteuliwa Kukaimu NSSF na Kisha 'Kutumbuliwa' ndani ya Masaa Matano - LEKULE

Breaking

6 Mar 2016

SSRA Yatetea Uraia Wa Dr Wangwe Ambaye Aliteuliwa Kukaimu NSSF na Kisha 'Kutumbuliwa' ndani ya Masaa Matano


Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) imetetea uraia wa Dk Carina Wangwe ikisema ni Mtanzania kwa kuandikishwa tangu mwaka 1999.

Dk Wangwe aliteuliwa juzi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama kuwa kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na kudumu katika nafasi hiyo kwa saa tano kabla ya uteuzi huo kutenguliwa kwa maelezo kuwa taratibu hazikuwa zimekamilika.

Kutenguliwa huko kulielezwa na baadhi ya watu kuwa ilikuwa ni kwa sababu mkuu huyo wa Tehama SSRA ni raia wa Uganda, madai ambayo yalikanushwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue,.

Taarifa ya ufafanuzi iliyotolewa jana usiku na Kitengo cha Mawasiliano cha SSRA, ilisema Dk Wangwe aliandikishwa kuwa raia baada ya kukidhi vigezo vya kuasiliwa (naturalisation) kwa mujibu wa kifungu cha 11 cha Sheria ya Uraia Na. 6 ya mwaka 1995.

Sambamba na hilo, taarifa hiyo ilisema Dk Wangwe aliukana uraia wa Uganda ikiwa ni pamoja na kurudisha pasipoti ya nchi hiyo aliyokuwa akiimiliki.

“Hivyo amekuwa raia wa Tanzania kwa kipindi cha miaka 17 na anamiliki cheti cha uraia Na. 58391 kilichotolewa na mamlaka husika tarehe 23 Aprili, 1999,” inasomeka taarifa hiyo.

Taarifa hiyo inasema Dk Wangwe ni mtumishi halali wa SSRA kuanzia mwaka 2011 hadi sasa baada ya kukidhi vigezo vya uraia na utaalamu.


“Ana uzoefu wa miaka 21 akiitumikia Tanzania katika nyadhifa tofauti ikijumuisha Chuo Kikuu Kishiriki cha Ardhi (miaka mitatu), Mfuko wa Pensheni wa PPF (miaka 9) na SSRA,” inasema taarifa hiyo. 

No comments: