Chadema Yaunda Chombo Kipya Cha Kulisimamia Jiji la Dar es Salaam - LEKULE

Breaking

6 Mar 2016

Chadema Yaunda Chombo Kipya Cha Kulisimamia Jiji la Dar es Salaam


Katika kile kinachoonekana kutaka kuliongoza Jiji la Dar es Salaam kwa mafanikio ya kupigiwa mfano, Chadema imeunda chombo kipya cha uongozi katika jiji hilo na kukiita ‘Uongozi wa Dar es Salaam Kuu’.

Pia, imemteua Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara kuwa mwenyekiti wa chombo hicho.

Chama hicho kikuu cha upinzani nchini kimeunda chombo hicho, huku kikieleza kuwa na uhakika wa kushinda uchaguzi wa meya wa jiji hilo kwa ushirikiano na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutokana na kuwa na idadi kubwa ya madiwani ikilinganishwa na CCM.

Uchaguzi huo umeahirishwa mara tatu na ya mwisho kwa kutumia zuio ‘batili’ la Mahakama na kuzua mtafaruku kati ya wabunge na wadiwani wa chama hicho dhidi ya polisi, jambo lililosababisha wabunge wawili, Halima Mdee na Waitara pamoja na madiwani watatu kufikishwa mahakamani wakidaiwa kumshambulia Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Theresia Mmbando ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi huo.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maazimio ya kikao cha Kamati Kuu jana, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema katiba ya chama hicho iliubadilisha Mkoa wa Dar es Salaam kuwa mamlaka ya kichama ya kimkoa na hivyo wilaya za Ilala, Kinondoni na Temeke zimepewa jina la mkoa badala ya wilaya.

“Baada ya kuona sintofahamu ya uchaguzi wa meya na namna ambavyo Serikali inavifanyia vyama vinavyounda Ukawa kuhusu suala hilo, chama kiliunda uongozi wa kimkoa, kimeamua kujipanga upya katika Jiji la Dar es Salaam,” alisema Mbowe.

Alisema wameunda chombo hicho kwa mujibu wa Ibara ya 6.1.3 ya katiba ya chama hicho ili kurejesha demokrasia iliyopotea katika Jiji la Dar es Salaam.

 Ibara hiyo inasema; Kwa kuzingatia ibara ya 6.1.2, ngazi ya juu ya chama itateua kamati ya muda itakayokuwa na wajibu wa kuratibu shughuli za chama na kuwaunganisha wanachama katika eneo lisilo na uongozi wa kikatiba mpaka watakapofikia uwezo wa kuwa na uongozi wa kikatiba.

Alisema kifungu hicho kinaongezewa nguvu na kifungu cha katiba cha 7.5.1 kinachoeleza jinsi ngazi za uongozi zinavyoundwa katika kila eneo la mkoa wa kiutawala wa Serikali Kuu, “Katika ngazi hii patakuwa na mikoa ya chama ambayo imetimiza masharti yaliyobainishwa na katiba na sehemu (c) inasema wilaya za Dar es Salaam zitakuwa na hadhi sawa ya kimkoa ya chama.”

Mbowe alisema mikoa hiyo ya kichama ya Kinondoni, Ilala na Temeke, itakuwa na chombo kitakachoiunganisha ambacho ni uongozi wa Dar es Salaam Kuu. 

“Uongozi huo umeteuliwa makusudi ili kuongeza nguvu, usimamizi na uratibu wa operesheni za chama katika jiji hili,” alisema. 

 Alisema chombo hicho kitakuwa na wajumbe wasiozidi 25 na uongozi wa chama hicho katika mikoa ya Kinondoni, Temeke na Ilala utabaki vilevile.

Mwenyekiti huyo wa Chadema alisema kamati inayounda chombo hicho itawahusisha wabunge wote wa kuchaguliwa na wa viti maalumu wa Chadema mkoani humo na mameya wa Ilala na Kinondoni.

Wabunge hao ni Mdee, John Mnyika (Kibamba), Waitara, Saed Kubenea (Ubungo), Susan Lyimo, Anatropia Theonist na Lucy Mollel.

Wengine ni mgombea wa Chadema katika nafasi ya umeya wa Jiji, Yesaya Mwita, Meya wa Ilala, Charles Kuyeko na Meya wa Kinondoni, Boniface Jacob pamoja na baadhi ya madiwani na viongozi wengine wa chama hicho jijini Dar es Salaam akiwamo Henry Kilewo ambaye ni Katibu wa Chadema Mkoa.


“Mwenyekiti wa kamati hii atakuwa Waitara na Makamu wake ni Bernard Mwakyembe ambaye ni diwani kutoka Wilaya ya Temeke. Katibu atakuwa Kilewo na Mweka Hazina ni Lyimo,”alisema Mbowe. 

No comments: