PLUIJIM ATOA YA MOYONI JUU YA USHINDI DHIDI YA APR - LEKULE

Breaking

14 Mar 2016

PLUIJIM ATOA YA MOYONI JUU YA USHINDI DHIDI YA APR


KIGALI


KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans Van Der Pluijm ameipongeza timu yake baada ya ushindi wa magoli 2-1 dhidi ya APR katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa wa Afrika uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa wa Amahoro Kigali, Rwanda.

Magoli ya Yanga yalifungwa na Juma Abdul katika dakika ya 20 na Thaban Kamusoko katika dakika ya 72, huku goli la kufutia machozi la APR likiwekwa kimiani na Patrick Sibomana katika dakika ya 92 ya mchezo.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali kutoka Rwanda, Pluijm amefurahishwa sana na vijana wake kuweza kuondoka na ushindi huo wa mabao 2-1 na kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele.

“Nimefurahi sana ila napenda kuwaambia wachezaji wangu lazima tuwe makini kuelekea mchezo wetu wa marudiano kwa sababu tumejua jinsi gani wapinzani wetu wanacheza na kwangu naona itakuwa mechi ngumu sana,” alisema.

Pluijm alisema hangependa kuongelea sana kuhusu wapinzani wake, lakini anachotaka kusema wapinzani wake wameonesha mchezo mzuri na sio timu ya kuibeza. “Mpira ni mchezo wa makosa wenzetu walifanya makosa na sisi tumeweza kuyatumia yale makosa waliofanya,” alisema.


Kwa upande wake Kocha Mkuu wa APR, Mtunisia Nizar Khanfir alisema wamepoteza mchezo kutokana na makosa waliofanya na waliweza kuadhibiwa kwa kufungwa 2-1. “Mechi bado ipo wazi inatakiwa tufanye bidii tushinde mechi yetu ya pili Jumamosi ijayo nchini Tanzania. Makosa tuliyofanya yanaweza kuepukika,ila nina imani kuwa tunaweza kufanya vizuri katika mechi yetu inayokuja,”alisema Kanifir.

No comments: