MKUU
wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda amesema kazi ya kuhakiki silaha
iliyoanza kwa wakazi wa Dar es Salaam, ilishaanza mkoani mwake takribani
miezi miwili iliyopita na kwamba ndiyo maana matukio ya kihalifu kwa
Arusha yamepungua.
Ntibenda
alisema hayo jana katika kikao cha Baraza la Ushauri la Mkoa wa Arusha
na kusema yeye ndiye mwanzilishi wa wazo la kilichoazishwa na Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda hivi karibuni.
Alisema
wakati wakisubiri kuapishwa katika viwanja vya Ikulu, Dar es Salaam
aliwaeleza wakuu wa mikoa jinsi alivyofanikiwa kudhibiti uhalifu kwa
kuwataka wakazi wa Jiji na mkoa wa Arusha kuhakiki silaha zao.
‘’Kazi
inayofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ni wazo
langu kwani sisi Arusha si mnaona uhalifu umepungua kwa asilimia kubwa
sana? Hiyo ni kwa sababu wengi wana silaha, lakini si mali zao,’’ alisema.
Akizungumzia
ulinzi, Ntibenda alisema hiyo inatokana na jitihada za kamati ya ulinzi
na usalama kuthibiti kwa kiasi kikubwa uhalifu na matukio yasiyokuwa na
amani na sasa Jiji la Arusha liko katika hali ya utulivu wa hali ya
juu.
Alisema
katika kipindi cha Januari mwaka jana hadi Desemba mwaka jana, jumla ya
magunia 270 ya bangi yenye uzito wa kilo 2,500 na ekari 25 za mashamba
ya bangi yaliteketezwa kwa kuchomwa moto.
Mkuu
huyo alisema operesheni hiyo ilifanyika katika vijiji vya Imbibya,
Ngarelaoni, Kisimiri Juu na Oldonyosambu na watuhumiwa 180 walikamatwa
na kesi 160 zilifikishwa mahakamani.
Akizungumzia
zuio la kutocheza `Pool’ saa za kazi, Ntibenda alisema wakuu wa wilaya
na wakurugenzi ni lazima washiriki kikamilifu kupiga vita mchezo huo
kuchezwa wakati wa kazi kwani ni jukumu la kila mmoja hapa na sio la mtu
mmoja mmoja.
No comments:
Post a Comment