Makonda Aingilia kati Vurugu za makanisani.....Asema Muumini Atakayekimbilia Polisi Kulishitaki Kanisa Atamuweka Rumande - LEKULE

Breaking

28 Mar 2016

Makonda Aingilia kati Vurugu za makanisani.....Asema Muumini Atakayekimbilia Polisi Kulishitaki Kanisa Atamuweka Rumande


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema mkoa wake hauko salama kama watu wanavyodhani kwa sababu silaha nyingi zinamilikiwa kiholela na mafunzo ya matumizi ya silaha hizo hutolewa hata kwa watoto.

Makonda alisema hayo jana wakati wa ibada ya Pasaka iliyofanyika katika Kanisa la Anglikana la Mtakatifu Albano na kuwataka wakazi wa Dar es Salaam kujitokeza kuhakiki silaha zao na kusalimisha zile zinazomilikiwa kinyume cha sheria.

Alisisitiza kwamba ifikapo Julai Mosi, operesheni maalumu ya kukamata silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria itaanza na yeye mwenyewe ndiye atakayeiongoza.

“Tumegundua kwamba kwenye bonde la mto unaotenganisha Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani, kuna mafunzo yanatolewa kwa watoto. Wazazi wanadhani watoto wao wamekwenda shule  kumbe wamechukuliwa huko.Hatuwezi kukubali hali hiyo iendelee."Alisema
Mkuu huyo wa mkoa aliwataka waumini waendelee kumuombea ili afanye kazi yake vizuri kwa kutenda  haki pia aliwataka pia wamwombee Rais Magufuli  kwa sababu kazi anayoifanya ni kubwa.
Alisema Rais anapotumbua jipu moja,ndani yake kuna kundi la watu wanaoathirika na hatua aliyoichukua hivyo, alisema watu wa aina hiyo hawawezi kumpenda kwa sababu amevunja mtandao wa masilahi yao.

“Ninaomba kanisa pamoja na viongozi wote wa dini mnisaidie katika kuhimiza suala la ulinzi na usalama ili amani yetu iendelee kudumu. Ninaomba tushirikiane katika hilo, Dar es Salaam haiko salama kama mnavyodhani, mengine siwezi kusema kwa sababu sijaruhusiwa na Rais,” alisema. 
Migogoro kanisani 
Akizungumzia migogoro makanisani, Makonda alisema hataki kusikia kiongozi yeyote wa dini anakimbilia polisi au mahakamani kutaka suluhisho la matatizo yao ya ndani na kuwa atamweka ndani atakayejaribu kufanya hivyo.

Alisema ni aibu kubwa kwa kanisa kukimbilia kwenye vyombo vya dola badala ya polisi na Serikali kukimbilia kanisani kuomba ushauri. Alisema kanisa ndicho chombo cha usuluhishi wa matatizo mbalimbali ya jamii.

“Serikali inahitaji msaada wa kanisa na viongozi wa dini ili iweze kufanya kazi vizuri. Sitaki kusikia polisi wanakwenda kanisani (kukamata watu) katika mkoa wangu na wale wanaotoa taarifa kutaka polisi nitawaweka ndani,” alisema Makonda ambaye kabla ya kuwa mkuu wa mkoa, alikuwa mkuu wa Wilaya ya Kinondoni.
 Askofu Mokiwa 
Awali, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Dar es Salaam, Valentino Mokiwa alibainisha mambo mbalimbali aliyoyaita majipu ambayo yanafanya kanisa hilo lisiendelee katika kufundisha waumini wake yaliyo mema.

Mokiwa alitaja mambo hayo kuwa ni pamoja na mashindano ya kimadhehebu. Alisema madhehebu mbalimbali yanashindanishwa kupima kanisa lipi ni kubwa, lina waumini wangapi, linamilikiwa na nani na nguvu yake ni ipi.


Jambo jingine alisema ni maaskofu wenyewe kupigana vita. Alisema sasa ni kawaida kwa askofu mmoja kumchimba mwingine, askofu mmoja kupanga mapinduzi dhidi ya mwingine na baadhi ya maaskofu kutukanana waziwazi. 

No comments: