Wahujumu uchumi, mafisadi na wote wanaokiuka viapo vyao wametakiwa
kujitumbua majipu wenyewe badala ya kusubiri Rais John Magufuli, kwa
kuungama kwa viongozi wao wa dini ili kusafisha nafsi zao.
Ushauri
huo ulitolewa juzi na Paroko wa Kanisa Katoliki mjini Mugumu wilayani
Serengeti, Alois Magabe wakati wa ibada ya mkesha wa Pasaka.
“Hawa
watu wanapaswa kumpata Mungu kwa kuungama kwa sababu matendo yao siyo
tu dhambi, bali yana madhara na udhalimu kwa umma kijamii, kiuchumi na
hata kisiasa,” alisema Padri Magabe na kuongeza:
“Matendo ya
uhujumu uchumi, ufisadi, wizi na ushirikina yanawatenga wanadamu na
Mungu, wahusika lazima watubu na kurejea katika njia safi badala ya
kusubiri kutumbuliwa na Rais,” alisema Padri Magabe.
Aliwataka
waumini wa dini na madhehebu yote kutumia maadhimisho ya sikukuu za
kidini kuhimiza matendo mema, kutimiza wajibu, haki, heshima kwa utu wa
mwanadamu na usawa kwa wote bila kujali tofauti miongoni mwao.
Naye
Askofu Naamon Kajeri wa Kanisa la Mennonite Tanzania (KMKT) Jimbo la
Mara, aliwataka viongozi wa Serikali na siasa ngazi zote kuongoza kwa
hofu ya Mungu, kutimiza kwa vitendo maandiko kuwa mamlaka zote duniani
zinawekwa na Mungu.
Askofu Kajeri aliwata wote wenye dhamana
kutenda haki na kuchukua hatua stahiki kwa wanaokiuka misingi, ili dhana
ya usawa isimame na kuonekana miongoni mwa wananchi.
Alisema kuendelea
kuhubiri dhana hiyo bila kuisimamisha, haina maana yoyote.
No comments:
Post a Comment